NA TIMA SALEHE,DAR ES SALAAM
Kocha msaidizi wa Simba Seleman Matola amesema mchezo wa leo wa Ligi Kuu ya dhidi ya JKT Tanzania utakuwa mgumu na wataingia uwanjani kwa kuwaheshimu.
Matola alisema JKT haijapata matokeo mazuri katika siku za karibuni lakini bado haiondoi ubora walionao hasa ukizingatia kikosi chao kinaundwa na wachezaji wengi wazoefu.
Matola ameongeza kuwa wataendelea kufanya mabadiliko ya kikosi mara kwa mara kutokana na ratiba kuwa ngumu hasa ukizingatia wanacheza kila baada ya siku mbili.
“Utakuwa mchezo mgumu lakini tumejipanga na tupo tayari kuhakikisha tunapata pointi tatu nyumbani. Mipango yetu ni kuhakikisha tunashinda kila mechi,” alisema Matola.
Kuhusu kuruhusu mabao, Matola alisema suala linawaumiza kichwa lakini wamelifanyia kazi mazoezini wakianza na mchezo wa leo
Kwa upande wake nahodha wa timu Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ alisema wachezaji wapo tayari kupambana kuhakikisha ushindi unapatikana.
“Kikubwa tunahitaji mashabiki wetu kujitokeza kwa wingi uwanjani kuja kutuunga mkono tunaamini tutapata ushindi,” alisema Zimbwe Jr.
Afisa Habari wa JKT Tanzania Masau Bwire alisema wamejipanga kuhakikisha wanawapa kichapo cha kizalendo wapinzani wao Simba.
Alisema kwa wale ambao hawafahamu namna ya kuwafunga wekundu hao wa msimbazi wawahi mapema uwanjani wakajifunze.