Skip to content

Simba,Yanga zahamishia mawindo Algeria 

NA CLEZENCIA TRYPHONE, Dar es Salaam

VIGOGO wa soka Tanzania Simba na Yanga wamepishana angani kila mmoja akiwa na msafa wake kwenda kuiwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa.

Simba inashiriki Kombe la Shirikisho huku Yanga wakicheza Ligi ya Mabingwa na kuanza vibaya mchezo wao wa kwanza, dhidi ya Al Hilal ya Sudan kwa kuchapwa mabao 2-0 katika uwanja wa Benjam Mkapa, wakati mnyama akitakata kwa bao 1-0.

Wawakilishi hao wameondoka jana Yanga wakielekea Algeria kukabiliana na MC Alger mchezo wa pili utakaopigwa Disemba 7 nchini humo.

Simba wao wanawafuata CR Costantine nchini Algeria mchezo utakaopigwa Disemba 8 nchini humo.

Wachezaji wa Yanga waliosafiri ni Bakari Mwamnyeto, Yao Kouassi,  Dickson Job,  Ibrahim Bacca,  Nickson Kibabage. Shadrack Boka na Kibwana Shomary, Khaleed Aucho, Mudathir Yahya,  Jonas Mkude, Clatous Chama, Duke Abuya,  Denis Nkane, Max Nzegeli,  Farid Mussa, Chekhan, Pacome Zouzoua, na Stephan Ki Aziz. 

Wengine ni Clement Mzize,  Jean Baleke, Kennedy Musonda na Prince Dube kikosi kitakachoenda kupambana katika mchezo huo.

Simba wao kikosi chao Mussa Camara, Ally Salim, Lionel Ateba,  Steven Mukwala,  Che Malone Fondoh,  Mohamed Hussein, Shomary Kapombe, Karaboue Chamou,  Abdulazack Hamza,  Valentin Nouma na Kelvin Kijiri.

Nyota wengine ni Mzamiru Yassin,  Debra Fernández,  Fabrice Ngoma,  Lazack Chasambi,  Agustine Okejepha,  Omary Omary, Edwin Balua, Kibu Denis, Jean Ahoua na Awesu.

Mkuu wa idara ya habari ya klabu ya Simba Ahmed Ally alisema wanakwenda kuhakikisha wanapambana bila ya kujali wako ugenini kikubwa ni matokeo mazuri waweze kujiweka katika sehemu nzuri.

Alisema michuano ina ushindani mkubwa hivyo kila mchezo ni kama fainali kwa upande wao.

Nahodha msaidizi wa Yanga Dickson Job alisema wanakwenda kupambana licha ya kuwa ugenini, kwani kila mchezaji ana ari  ya kupata ushindi.

“Tulipoteza mchezo wa kwanza nyumbani ndio mpira ulivyo tunaenda ugenini tukiwa na nguvu kubwa ya kuhakikisha tunapata pointi tatu muhimu,”alisema.

Meneja wa habari na mawasiliano wa Yanga Ally Kamwe,alisema  wanakwenda  kwa tahadhari  na lazima wakapambane kwani mchezo utakuwa mgumu.

Alisema wanakwenda kusaka pointi tatu na wakikosa hizo basi wpate sare na sio kufungwa.

Wakati huo huo mlinda mlango wa klabu ya Simba Aish Manula ameshindwa kuendelea na safari ya Algeria baada ya kupata changamoto ya kiafya akiwa uwanja wa ndege hapa jijini.

Manula alikuwa sehemu ya wachezaji waliotangazwa na Simba kwenda Algeria kwa ajili ya mchezo wa pili wa makundi ya kombe la Shirikisho dhifi ya CR Costantine Disemba 8.

Kwa mujibu wa taarifa ya Simba iliyotolewa muda mchache kabla ya safari ilibainisha kuwa Manula alipokuwa uwanja wa Mwalimu Julius Nyerere alipata tatizo la kiafya lililomfanya ashindwe kuendelea na safari na kulazimika kusalia Dar es Salaam.