Skip to content

Soraga: Mabalozi utangazeni utalii kimataifa

NA KHAMISUU ABDALLAH

WIZARA ya Utalii na Mambo ya Kale, imesema itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha utalii wa Zanzibar unaendelea kupata hadhi ya kimataifa na kuchangia kikamilifu katika uchumi.

Waziri wa wizara hiyo, Mudrik Ramadhan Soraga, alieleza hayo mara baada ya kukabidhi cheti kwa mabalozi wanne wa heshima, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa wizara hiyo Kikwajuni.

Alisema uteuzi wa mabalozi hao umefanyika kwa kuzingatia uwezo wao wa kufikia watu wengi na anaamini kuwa watautangaza utalii wa Zanzibar kitaifa na kimataifa kwa kutumia mbinu bora za kisasa.

“Wizara imejiridhisha kuwa mabalozi hawa watatumia majukwaa yao ya kijamii na nafasi walizonazo katika jamii kuhamasisha utalii na kutoa elimu kuhusu vivutio vya kipekee tulivyonavyo kama taifa,” alisema.

Waziri Soraga aliwataka wananchi na wadau wa utalii kuwapa ushirikiano mabalozi hao ili kufanya shughuli zao kwa ufanisi na kuiletea Zanzibar maendeleo.

Naye Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Aboud Suleiman Jumbe, alisema wanatarajia mabalozi hao kuwakilisha vyema katika kutumia utalamu na uzoefu wao kwenye kuvutia watalii wengi zaidi kufika Zanzibar na kufurahia bidhaa pekee za kitalii zilizopo.

Alizitaja miongoni mwa bidhaa hizo ni bahari, fukwe, urithi wa kihistoria, utamaduni, mambo ya kale, michezo, mikutano na utalii wa chakula.

“Tunawaomba mabalozi wateule kutusaidia kwa nguvu zote kuitangaza Zanzibar kwa kutumia mbinu bora na za kisasa katika nyanja za kimataifa ili kutimiza malengo yetu ya kukuza sekta ya utalii,” alisema.

Aidha aliwataka mabalozi hao kuitangaza Zanzibar na kupitia mifumo mbalimbali ya habari, maelezo, taarifa na matangazo ya kibiashara na kutumia vyombo vya habari vya ndanii na kimataifa kufikisha ujumbe kwa jamii kuhusu utalii wa Zanzibar.

Aliwasisitiza kutumia uzoefu na utalamu wao wa kisekta kutoa simulizi nzuri na za kuvutia kuhusu visiwa vya Zanzibar, watu wake, utamaduni wake na vivutio kwa ujumla.

Jumbe alibainisha kuwa vitu hivyo ndivyo vinavyoipa umaarufu Zanzibar kama kimbilio kuu la watalii ukanda wa Afrika Mashariki na kuipeleka Zanzibar sehemu ya ushindani kimataifa katika sekta ya utalii.

Alisema fursa nyingine ambao mabalozi hao wanayo ni kukutana na wawakilishi wa kimataifa ili kuwezesha kutumia mitandao ya mawasiliano na mbinu za kisasa katika kuitangaza Zanzibar kiutalii.

“Lakini pia moja ya majukumu muhimu kwa mabalozi hawa ni kuutangaza utalii wa Zanzibar kwa kuzingatia sura muhimu ya kibinadamu na kiutu, hii inahusisha ukarimu wa watu wa Zanzibar hivyo kuionesha dunia kuwa ni kisiwa cha furaha na ukarimu wa pekee”, alisema.

Akizungumza kwa niaba ya mabalozi wenzake, Ruqaiya Ahmed Karanja, alisema sekta ya utalii ni inagusa uchumi, ajira na muonekano mzima wa Zanzibar kimataifa.

“Fursa tuliyoipata ni ya kipekee na tutahakikisha tunaitumia fursa hiyo kukuza sekta utalii nchini ili kuendelea kuchangia pato la taifa”, alisema.

Aliahidi kuifanya Zanzibar kung’ara duniani kupitia sekta ya utalii na kuitangaza katika uwekezaji na urithi wa kimataifa.

Mabalozi wengine ni Aloes Inninger, Dk. Lisa Wana Xiangune na Abdulrahim Abdulhamid Numa.