WAZIRI wa Habari, Vijana,Utamaduni na Michezo, Tabia Mauli Mwita, amewaomba vijana kubeba jukumu la kulinda amani ili kuhakikisha wanapata maendeleo na kuhakikisha usalama wa vizazi vyao hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam katika siku ya pili ya kongamano la kitaifa la ajenda ya amani na usalama wa vijana sambamba na kuadhimisha siku ya amani duniani lililomalizika jana katika Kituo cha Mikutano Kimataifa cha Julius Nyerere (JKCI).
Alisema vijana wanatumika kisiasa badala ya kutumika kwa mambo yenye manufaa kwao, hivyo wana wajibu wa kuhakikisha wanalinda amani na kusimamia ajenda zao.
“Muda mfupi ujao, Tanzania bara itakabiliwa na uchaguzi wa serikali za mitaa, nawaomba vijana kufikisha ujumbe wa amani kwa vijana wengine na msikubali kuwa ngazi ya kupanda watu na kuonekana wao huku nynyi (vijana) mkibaki nyuma,” alisema.
Aidha, aliwataka vijana wenye sifa kujitokeza kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi huo na wakati wa kufanya hivyo ni sasa.
“Kila mwenye sifa na uwezo agombee nafasi katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwani vijana mnaweza, viongozi wetu wamekuwa wakitoa kipaumbe kwa vijana wenye uthubutu kwa hivyo tumieni fursa hii,” alisema.
Aliwaomba kuondoa woga bali waongeze uthubutu wa kushiriki kikamifu katika chaguzi za serikali za mitaa ili watimize lengo la kikatiba la kuchagua ua kuchaguliwa.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Zuhura Yunus, alisema suala la amani linaanzia katika ngazi ya familia kwani kama familia haina amani hakuna jambo linaloweza kufanyika.
Alifafaniua kuwa iwapo familia zitajenga misingi inayoegemea haki, umoja na ushirikiano kuna uwezekano mkubwa wa amani kuimarika katika jamii hicvyo aliwataka washiriki wa kongamano hilo kuwa mabalozi wa kuilinda badala ya kushiriki kuibomoa.
Akifungua kongamano hilo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko, aliwahimiza vijana kubeba agenda ya amani na maendeleo kwa kuzingatia kaulimbiu ya kongamano hilo isemayo ‘Kijana chukua hatua kudumisha utamaduni wa amani Tanzania’.
Kongamano hilo la siku tatu lilifanyika sambamba na utoaji wa elimu katika skuli mbali mbali kuhusu utamaduni wa amani kupitia midahalo ya vijana na mbio za amani katika mikoa ya Tanga, Mjini Magaribi Unguja, Pwani, Lindi na Mtwara ambapo zaidi ya vijana 10,000 walifikiwa lilifungwa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Jakaya Kikwete.