Skip to content

Tabia:Michezo yote kipaumbele cha Serikali

NA MWANDIHI WETU

WAZIRI wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita amesema Serikali inathamini michezo yote na sio mpira wa miguu pekee.

Tabia aliyasema hayo huko Mtoni KVZ, wakati wa sherehe ya kuipongeza timu ya Netiboli ya KVZ (KVZ Queens),baada ya kufanya vizuri katika kombe la Muungano, lililofanyika Jijini Dar-es-Salaam hivi karibuni.

Alisema Serikali inaendelea kujenga viwanja vya michezo ili wanamichezo waweze kushiriki michezo ya aina zote.

Alisema wizara itaendelea kupanga mikakati ya kuhakikisha timu hiyo na nyengine zinaendelea kushinda katika mashindanoyanayofanyika ndani na nje ya nchi ili kuipa hadhi Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Hata hivyo amewataka wanamichezo wa Zanzibar kufanya mazoezi kwa bidii na kudumisha nidhamu ili waweze kushinda mashindano yote yanayoandaliwa.

Mbali na hayo Tabia ameahidi kusaidia vifaa mbalimba vya michezo ikiwemo jezi, mipira na soksi ili kuunga mkono kazi kubwa inayofanywa na timu hiyo.

Mkuu wa Kikosi cha KVZ Meja Said Ali  Shamuhuna alisema kitendo cha timu hiyo kuchukua kombe hilo, ni jambo kubwa na kimetoa heshima kwa kikosi hicho.

Alisema kwa upande wa Netiboli kwa sasa hawana wasiwasi sana, wanajiandaa zaidi na mashindano ya Afika Mashariki yanayotarajiwa kufanyika Zanzibar, lakini kwa sasa wanajipanga zaidi kwa mchezo wa mpira wa miguu na michezo mengine.

Katibu wa michezo KVZ kepteni Hassan Omar alisema timu hiyo, imefanikiwa kushinda mechi zote iliocheza na kutangazwa kuwa bingwa wa mashindano hayo mwaka 2024.

Mashindano hayo, yaliofanyika Jijini Dar-es-salaam, yamezishirikisha timu saba (7) tano kutoka Zanzibar na mbili (2) kutoka Dar-es-Salaam ambapo wachezaji wa timu hiyo ambao ni askari wa KVZ wamepandishwa vyeo na wachezaji ambao ni raia wamekabidhiwa fedha taslim.

Miongoni mwa timu saba (7) zilizoshiriki katika Kombe hilo kutoka Zanzibar ni pamoja na KVZ, Mafunzo, JKU, Zimamoto na Afya wakati kutoka Dar-es-Saalam ni Uhamiaji na Magereza.