NA MWANDISHI WETU
KURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Gissima Nyamo-Hanga amesema TANESCO inathamini michango inayotolewa na washirika wa maendeleo katika kuimarisha sekta ya nishati nchini.
Aliyasema hayo Mombasa nchini Kenya wakati akiwasilisha mada kuhusu sekta ya umeme Tanzania katika mkutano uliowakutanisha nchi wanachama wa EAPP na wadau katika sekta ya umeme.
“Tunatambua ushiriki wa washirika wa maendeleo katika kuongeza biashara ya umeme nchini Tanzania kwa kufadhili miundombinu ya mfumo wa umeme katika maeneo ya uzalishaji na mifumo ya usambazaji,” alisema.
Kuhusu wawekezaji binafsi katika sekta ya umeme, alisema wapo wawekezaji na kutanabaisha kuwa kwa sasa hakuna wawekezaji binafsi kwa upande wa usambazaji umeme na kwa mfumo wa usafirishaji umeme unaendeshwa na serikali kupitia TANESCO.
Aliongeza kuwa, serikali inaendelea kuangalia njia bora ya kushirikisha sekta binafsi katika ujenzi nauendeshaji mifumo ya usafirishaji wa umeme bila kuathiri uthabiti wa mifumo hiyo.
Akielezea faida zitakazopatikana kutokana na Tanzania kushiriki soko la kanda la biashara ya umeme kwa kuingia katika muunganiko wa kuuziana na kununua umeme kwa upande wa Mashariki (EAPP) na Kusini mwa Afrika (SAPP), alisema nchi itafaidika kwa kuuza umeme kutokana na uwekezaji mkubwa serikali inaoufanya katika eneo la uzalishaji.
Alisema kijiografia Tanzania ipo katikati ya nchi zilizo upande wa kaskazini mwa Afirika zitakapohitaji kufanya biashara ya umeme na nchi zilizo kusini mwa Afrika na zitahitajika kuupitisha umeme katika miundombinu ya kusafirishia umeme ya Tanzania hivyo nchi itafaidika kwa kupata fedha za kigeni.
Alisema kwa upande mwingine kutakuwa utulivu wa gridi kupitia kuunganishwa kwa gridi ya kanda kwa karibu.