NA FATMA KITIMA, DAR ES SALAAM
MKURUGENZI mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika, Dk. Faustine Ndugulile (55), amefariki dunia, miezi kadhaa baada ya kuchaguliwa katika nafasi hiyo.
Dk. Ndugulile, mbunge na daktari, alifariki Jumatano asubuhi nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu, Spika wa Bunge la Tanzania alisema.
Agosti mwaka huu, alichaguliwa kuwa mkuu wa kanda wa WHO, kuchukua nafasi ya Dk. Matshidiso Moeti raia wa Botswana, ambaye amehudumu kwa mihula miwili ya miaka mitano.
Alipaswa kuchukua nafasi hiyo Februari mwaka ujao.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema “ameshtushwa na kuhuzunishwa sana” na kifo cha Ndugulile.
Rais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu pia alituma salamu za rambirambi kwa familia ya mbunge huyo, Spika wa Bunge na wabunge.
Ugonjwa ambao alikuwa akitibiwa haujawekwa wazi.
Kabla ya kuchaguliwa katika wadhifa wa WHO, Ndugulile alikuwa na taaluma ya kipekee katika siasa na afya ya umma.
Aliwakilisha jimbo la Kigamboni jijini Dar es Salaam kama mbunge na kushika nyadhifa kadhaa muhimu kiserikali, ikiwamo Naibu Waziri wa Afya na baadae Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Aliteuliwa kushika wadhifa wa wizara ya afya mwaka 2017 na kuhudumu katika nafasi hiyo hadi alipoondolewa na Rais wa awamu ya tano, marehemu Dk. John Pombe Magufuli Mei 2020, huku kukiwa na kilele cha janga la virusi vya ugonjwa wa UVIKO-19.
Hakukuwa na sababu zilizotolewa za kufutwa kwake kazi, ingawa ripoti za vyombo vya habari zilidai ni kutokana na msimamo wake juu ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 nchini.
Bungeni na kwingineko, Ndugulile mara kwa mara alipigwa picha akiwa ameziba mdomo na pua kwa kutumia maski.
Lakini mwanzoni mwa muhula wake wa pili madarakani, Disemba mwaka huo huo, Rais Magufuli alimteua Ndugulile kuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Ndugulile alishika wadhifa huo hadi kifo cha Magufuli mwaka 2021.
Kabla ya kujiunga na siasa mwaka 2010, Ndugulile aliwahi kuwa Mkurugenzi katika Wizara ya Afya akisimamia huduma za uchunguzi.
Alichukua jukumu muhimu katika kuanzisha huduma ya kitaifa za damu salama mnamo 2006, ambapo alihudumu kama Meneja mwanzilishi wa program hiyo.
Pia alifanya kazi katika vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Maradhi (CDC) nchini Afrika Kusini.
Tanzania ilimpendekeza kushika wadhifa wa WHO mapema mwaka huu, kutokana na uzoefu wake na kujitolea kwake katika masuala ya afya duniani.
Baada ya kuchaguliwa mwezi Agosti, alieleza kujitolea kwake kuendeleza afya katika bara hilo.
“Ninaahidi kufanya kazi nanyi na ninaamini kuwa kwa pamoja tunaweza kujenga Afrika yenye afya,” alisema wakati huo.
Kwa upande wake, Diwani wa Msasani, Luca Neghesti, amesema amepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Ndungulile akisema ni pigo kubwa kwa Watanzania.
Alisema alikuwa mtu wake wa karibu na kwamba kifo chake kimetokea katika kipindi ambacho alikuwa anahitajika kwa maendeleo ya sekta ya afya Afrika.
“Ni kazi ya Mungu, hatuwezi kuelewa kwa nini imetokea bali ni kumuombea ndugu yetu awe na nafasi nyepesi mbele ya haki na Mwenyezi Mungu ampokee apumzike kwa amani,”alisema
Alisema Dk.Ndungulile alikuwa kiongozi wa watu, shupavu, msikivu namtu mwenye maono ya mbali na mpenda maendeleo.