Skip to content

TRCA kuendeleza elimu kukabili utapeli mitandaoni

  • Zanzibar

NA MWANAJUMA MMANGA

MENEJA wa Ofisi ya Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) ofisi ya Zanzibar, Esuvatie-Aisa Masinga, amesema wataendelea kutoa elimu kwa makundi mbali mbali ili kukabiliana na changamoto ya utapeli mitandaoni unaondelkea kuongezeka kila siku.

Akizungumza wakati wa mafunzo ya siku moja kwa wazee wa mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni ya ’Ni rahisi sana’ inayoendeleshwa na TCRA yaliyofanyika katika ukumbi wa ZSSF Kariakoo, mjini Unguja.

Alisema kukua kwa teknolojia kumeongeza matishio ya kiusalama mitandaani na kusababisha changamoto mbali mbali huku wazee wakiwa waathirika wakuu hivyo mafunzo hayo yatawasaidia kujua njia za kuilinda pamoja na kutambua viashiria vya utapeli na uhalifu mwengine kabla haujatokea.

Aidha alieleza kuwa kuptia kampeni hiyo, jamii itatambua hatua za kuchukua ikiwa ni pamoja na kutuma taarifa kupitia namba zilizowekwa na mamlaka hiyo ili kuwabaini watu wanaojihusisha na vitendo hivyo.

“Hivyo wazee wangu nawaomba muendelee kujilinda wenyewe na kukataa kumpa mtu yoyote namba yako ya siri (pass word) ili kuepusha kutapeliwa”, alieleza Masinga.

Aliongeza kuwa kati ya mwezi Juni na Septemba, mwaka huu katika mkoa wa Mjini Magharibi pekee jumla ya laini 518,058 zilisajiliwa na majaribio ya ulaghai 122 yaliripotiwa idadi aliyoeleza ni kubwa ikilinganishwa na mikoa mingine.

“Kwa upande wa mkoa wa Kaskazini Pemba, laini 124,684 zilisajiliwa na majaribio 84 ya ulaghai yaliripotiwa wakati katika mkoa wa Kusini Pemba laini zilizosajiliwa zilikuwa 124,472 na kulikuwa na majaribia10 ya ulaghai”, alifafanua Mkurugenzi huyo.

Aliendelea kufafanua kuwa katika mkoa wa Kusini Unguja, laini zilizosajiliwa 110,970 huku matukio sita ya ulaghai yaliripotiwa na kwa mkoa wa Kaskazini Unguja laini 73,743 zilizosajiliwana majaribio 12 ya uhalifu yaliripotiwa.

Naye Mkuu wa Divisheni ya Pencheni Jamii na Maendeleo ya wazee kutoka Idara ya ustawi wa jamii na wazee ndani ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bikame Sheha Ussi, alisema mafunzo hayo yamewapa faraja kwani ukizingatia mazingira ya sasa kumekuwepo utapeli kwa wananchi mbalimbali na kusema kuwa wazee wamekuwa wakitapeliwa na kusababisha vifo kwa wazee.

Alisema mafunzo hayo, yamesaidia kujikinga na utapeli pamoja na kuwa wajumbe kwa wenzao na hata kwa watoto wao pamoja na kuwapongeza viongozi wa TCRA kwa kuwafikishia mafunzo hayo ambayo yamekuwa na umuhimu mkubwa na kuwataka kuendelea kutao mafunzo hayo kwa rika jengine.

Mmoja wa wazee walioshiriki mafunzo hayo, Juma Ali Haji, alisema yamewapa dira nakuwasaidia kupata njia za kukabiliana na changamoto mbali mbali za matumizi mabaya ya mitandao.

Mzee haji alieleza kuwa masuala ya utapeli yamekuwa yakiwakabili ambapo matapeli amekuwa wakitumia mbinu mbali mbali hivyo wameliomba jeshi la polisi na TCRA kuendelea kuwakamata pamoja na kutoa elimu kwa umma kutumia simu za mkononi.