UBALOZI wa India nchini Tanzania, umefanya mazungumzo na mabalozi kutoka nchi mbalimbali za Afrika zenye uwakilishi nchini, kuhusu matumizi ya akili mnemba (AI) katika diplomasia, yaliyohusisha maprofesa mashuhuri kutoka Taasisi ya Teknolojia ya India (IIT) Madras.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na wanadiplomasia na maofisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar,. Mwanakhamis Adam Ameir, aliwaeleza wanadiplomasia hao kuhusu mkakati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kuiweka IIT Madras Zanzibar kuwa kitovu cha elimu barani Afrika.
Aliwaomba mabalozi kutembelea taasisi hiyo na kuhimiza uandikishaji wa wanafunzi kutoka nchi zao kwa ajili ya elimu ya juu.
Kwa upande wake, Balozi wa Muungano wa Comoro na Mkuu wa Mabalozi, Dk. Ahamada El Badaoui Mohamed Fakih, alipongeza uanzishwaji wa programu hiyo akisema ni muhimu katika ulimwengu wa sasa huku akisifu juhudi za kupunguza mgawanyiko wa kidijitali barani Afrika.
Nae Prof. Raghunathan Rengaswamy, Mkuu ya kimataifa wa IIT Madras, alitoa maarifa juu ya matumizi ya akili mnemba katika uhusiano ya kimataifa na diplomasia, ikitoa mtazamo wa kipekee juu ya ushawishi wa teknolojia katika diplomasia.
Mkurugenzi wa IIT Madras Zanzibar, Prof. Preeti Aghalayam, aliwaeleza washiriki juu ya fursa za kielimu zinatolewa na taasisi hiyo kwa wanafunzi wa Afrika na jinsi ya kutumia fursa katika fani zinazochipukia kama vile akili mnemba, sayansi ya data na miundombinu ya bahari, zinazotolewa katika chuo hicho.
Aidha, alieleza fursa zilizopo kwa wanafunzi wa Afrika, faida za kusoma katika taasisi hiyo na utaratibu wa udahili.
Alisema uandikishaji katika programu za akili mnemba, sayansi ya data na miundo ya bahari, huanza katikati ya Januari kila mwaka.
Charles Kamoto, Mkurugenzi Mkuu wa Airtel Tanzania, alizungumzia ushiriki mpya wa program ya Airtel Africa Fellowship iliyozinduliwa kwa wanafunzi wa taasisi hiyo na mipango kama hiyo ya Airtel katika kuendeleza ubora wa elimu na ubunifu wa kidigitali barani Afrika.
Balozi wa India nchini Tanzania, Bishwadip Dey, alisisitiza upekee na umuhimu wa tukio hilo, akisema akili mnemba ni uwanja mpya unaojitokeza unaostahili kuzingatiwa.
Alisema AI ina jukumu muhimu katika michakato ya uchambuzi wa kufanya maamuzi na kukuza uelewa wa kina wa mienendo ya kimataifa.
Aliwashukuru mabalozi wenzake na wanadiplomasia wengine kwa kushiriki kwa wingi majadiliano hayo.
Nao washiriki, walieleza kuwa tukio hilo lilikuwa la kuelimisha na kunufaisha, huku wakiwa na shauku kubwa ya kutafuta fursa za kushirikiana na IITM Zanzibar katika uwanja huo.