MOJA ya kivutio cha kupendeza kilichopo katika mji wa Zhengzhou ni mto manjano, ambapo kwa kihichina mto huo unajulikana kama Huwang He ama ‘yellow river’.
Katika mji wa Zhengzhou, mto manjano unapatikana upande wa kaskazini- magharibi ukikatiza urefu wa kilomita 20 katika mji huo unaopatitikana katika jimbo ya Henan linaloelezwa kuwa lina ustaarabu wa kale wa utamaduni wa kichina.
Taarifa zinaeleza kuwa mto manjano ama ‘yellow river’ ni mto wa pili kwa ukubwa nchini China na mto wa sita kwa urefu duniani.
Sababu za kuitwa mto manjano, inatokana na rangi ya maji inayotokana na matope.
Una urefu wa kilomita mnamo 5,400 ukielezwa kuanzia nyanda za juu za Tibet hadi delta ya bahari ya Bohai ambayo ni sehemu ya bahari ya Mashariki ya China.
Kabla ya kufika baharini, mto unapita katika eneo la tambarare ya China Kaskazini ambako ustaarabu wa China ulianzishwa. Ndiyo sababu mto manjano umeitwa mara nyingi mto mama wa China na chanzo cha ustaarabu wa Kichina.
Kwa muda mrefu wakulima nchini China walitumia maji ya mto huo kwa ajili ya kilimo na hivyo kusababisha madhara ya uharibifu mkubwa wa mazingira.
Ili kunusuru hali ya mazingira yaliyochafuliwa na wakulima, Rais wa China Xi Jinping alifanya ziara katika mji wa Zhengzhou na kuagiza hatua zichukuliwe za kuhifadhi mazingira ya mto huo.
Katika maagizo hayo, Xi alisema uhifadhi wa mazingira ndio uhakika wa kulinda maisha na viumbe wakiwemo wanaadam, hivyo lazima mazingira katika mto huo yahifadhiwe na yalindwe.
Agizo hilo la Rais Xi Jinping lililazimisha kuchukuliwa hatua za haraka za kuhifadhiwa bonde la mto huo katika mji wa Zhengzhou ambapo mamlaka ililazimika kuwahamisha wakulima na kuwapatia kazi mbadala ili jukumu la kuhifadhi wa mazingira litekelezwe.
Ukipata fursa ya kulitembelea bonde na mto manjano katika mji wa Zhengzhou, hivi sasa ni eneo la mfano bora duniani la utunzwaji na uhifadhi wa mazingira na ni miongoni mwa vivutio vizuri mno vya utalii.
Ukitembelea kwenye ufukwe wa mto huo utashuhudia uzuri wa uhidhi wa mazingira na kuwa eneo zuri la kivutio cha utalii na huwezi kuamini kwamba wakulima katika eneo hilo waliliharibu kwa kuchafua mazingira.
Mamlaka za mji wa Zhengzhou zimechukua hatua ya kupanda miti na kulirejesha kwenye uasili wa mazingira eneo hilo lenye hewa safi ya Oxygen.