NA KHAULAT SULEIMAN, SUZA
WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Leila Mohamed Mussa amesema, kujengwa viwanja vya michezo vitasaidia kuleta mageuzi na kuibua vipaji kisiwani Pemba .
Aliyasema hayo katika hafla ya ufunguzi wa mradi wa ujenzi wa viwanja vya mpira katika skuli ya sekondari Mchangamdogo wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Alisema mtaala wa elimu ya michezo utasaidia kwa asilimia kubwa kutoa watalamu na vipaji mbali mbali kutoka skuli na hata mitaani kwa kuwajengea uwezo wa kitaalamu ili kuleta mabadiliko katika sekta ya michezo.
Alieleza kuwa ni jukumu la kila mzazi kuhakikisha anatoa ushirikiano kwa walimu na watoto,kwa kuachana na dhana mbaya ya kuwa michezo ni uhuni na kupoteza muda.
Mkuu wa wilaya ya Wete Hamad Omar Bakar aliwataka wanafunzi na walimu kukihifadhi kiwanja hicho pindi tu watakapokabidhiwa mara baada ya kukamilika.
Afisa Mdhamini Wizara ya Habari, Utamaduni, na Michezo Pemba Mfamau Lali Mfamau alieleza kuwa, viwanja hivyo viwe sehemu ya kuunganisha watu wala wasibaguane kwa kuweka makundi, kwani watu wote wana haki ya kushiriki katika michezo.
Mwakilishi kutoka Shirika la Ujerumani Luis Scheuber alieleza kuwa Serikali ya Ujerumani kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ipo tayari katika ujenzi wa viwanja ya michezo Unguja na Pemba
Mwalimu mkuu wa skuli ya Sekondari Mchangamdogo Maryam Haji Othman aliishukuru wizara kwa kushirikiana pamoja na kujengewa kiwanja cha michezo kwa lengo la kuwajengea uwezo katika masuala ya michezo.