WATU wengi wamekuwa wakifundishwa na kuelewa kwamba tunachotakiwa kuwa nacho ili tuishi kwenye ndoa ni upendo peke yake, upendo ukiwepo basi hakuna haja ya kingine chochote, mengine yatakuja wenyewe.
Hiyo ni nadharia potofu na wengi kwa kushindwa kuelewa wamepata shida sana kwenye ndoa zao. Hapa ninakupa nguzo nyingine muhimu zinazosaidiana na upendo katika kuidumisha ndoa au mapenzi yoyote.
Yafuatayo ndio mambo yanayoweza kuleta mafanikio katika ndoa.
UFAHAMU – Kwa kuwa na ufahamu mkubwa. Ndoa inaweza ikajengwa kwa kufahamu sababu ya nyinyi kuwa pamoja, ufahamu wa mambo yapi myazingatie kwenye ndoa yenu.
Nini mfanye na nini msifanye, yapi mambo hatari na yapi sio hatari. Je unamfahamu mwenzako kwa kiasi gani na je unafahamu nini utegemee kwa jinsia aliyonayo?
UELEWA – Ni busara kuelewa mambo ya mahusiano kabla ya kufunga ndoa. Unapaswa kuelewa tabia ya rafiki yako, nguvu na udhaifu wake.
Kuna vitu kwenye ndoa havihitaji majibizano yasiyo lazima, vinahitaji tu uelewa, ukiwa muelewa utapunguza misuguano isiyolazima, elewa haraka kile mwenza wako anachotamani umuelewe, penye kuhitaji suali basi uliza ueleweshwe. Usijifanyishe umeelewa wakati haujaelewa.
HEKIMA– Hekima ni muhimu kwenye ndoa. Hii inakuwezesha katika kuamua vizuri kwa ustawi wa ndoa yako. Ni hekima ndio inakusaidia kufanya maamuzi yasiyo na majuto. Maamuzi ambayo yatazingatia ufahamu wako na uelewa wako.
MAPENZI/UPENDO – Mapenzi yanapaswa kuwa jambo la nne la ndoa yenye mafanikio na sio la kwanza. Unapokuwa na uelewa, ufahamu na hekima basi upendo unakuja kuketi au kutuama sehemu salama kabisa. Ukiwa na upendo na hivyo vingine havipo basi utashangaa misuguano haishi.
Msisitizo: Ni vizuri ukajiuliza kabla ya kufunga ndoa “Ni kwa nini unafunga ndoa? “Nisababu zipi zinanifanya niingie kwenye ndoa?” usipojiuliza suali hili mapema na kulipatia majibu ya kiufasaha basi baada ya kuoa au kuolewa unaweza kuja kujiuliza “Ni kwa nini nilifunga ndoa?” “Hivi kwanini nilioa au niliolewa?”. Bahati mbaya sana wakati unajiuliza masuali haya utakuwa umechelewa.
Ili kuwa na ndoa yenye mafanikio unahitaji ngazi tatu za mahusiano
Ngazi ya kwanza ya mahusiano ni Mungu/muumba. Hii ndio ngazi ya kwanza ya uhusiano na yenye umuhimu mkubwa sana, ngazi hii itaamua kiasi kikubwa cha uhusiano wako na wengine.
Kumshirikisha Mungu katika kila tamanio la moyo wako. Zungumza na Mungu ni aina gani ya mume au mke unahitaji. Ni aina gani ya familia unayoitamani.
Kuwa mwaminifu kwa Mungu kumwambia kila kitu kuhusu mume wako/ mke wako, mwambie kuhusu unachopendelea kama vile rangi, tabia, ngazi ya elimu na mengine yanayohusiana na hayo.
Wengi wetu husahau ngazi hii halafu tunapoingia kwenye ndoa kwa kukurupuka tunajikuta vitu vingi sivyo tulivyowahi kutamani na wala havikuwahi kuwa ndoto yetu hapo ndio kukata tamaa huja kwa kasi na kiu ya kutoka kwenye hiyo ndoa huanza.
Ndoa nyingi sana zimevunjika kwa staili hii. Tafiti zinasema wanandoa wenye mahusiano binafsi mazuri na Muumba wao huweza kuelewana, kuthaminiana na kuheshimiana kwa urahisi zaidi kuliko wale wasio na uhusiano huu.
Ngazi ya pili ya mahusiano ni familia
Familia ni muhimu sana wakati wa kutafuta mchumba. Uhusiano wa familia wenye nguvu utakusaidia kufanya maamuzi mazuri. Kwanini maamuzi mazuri ni muhimu?
Hii ni kwa sababu, kuna tofauti kati ya maumivu kabla ya ndoa na maumivu ya kwenye ndoa. Ni bora ukaifahamu familia ya huyo mpenzi wako kwa kina ili kupunguza maumivu ya badaye.
Bora uumie sasa hivi kwa vile utakavyovigundua kuhusu yeye au familia yako kuliko kuvinyamazia halafu vikakuletea maumivu makubwa kesho ukiwa kwenye ndoa tayari.
Hakikisha unaifahamu familia ya rafiki yako, jua mahusiano yake na wazazi wake na ndugu zake. Chunguza kama wana magonjwa ya kurithi, chunguza kama kunatabia za kifamilia, chunguza wazazi na ndugu wanavyomchukulia yeye, angalia ushirikiano wao katika mambo ya kifamilia, chunguza mambo yahusuyo imani zao pia.
Fahamu yeye ni mtoto wa ngapi na wako watoto wangapi na wajinsia gani, taarifa hizi zitakusaidia sana katika maisha yako ya ndoa.
Ngazi ya tatu ya mahusiano ni marafiki
Unaweza kuwa na marafiki wa karibu kuliko ndugu, lakini marafiki hao wanaweza kukushawishi vizuri au vibaya.
Utakayefunga nae ndoa anaweza kutoka miongoni mwa marafiki zako, hivyo marafiki wabaya wanaweza kukusababishia ukapata mwenzi mbaya.
Utakayefunga nae ndoa anaweza kubadilisha tabia zako na hata kukufanya uwabadili marafiki zako, marafiki wanaokuzunguka pia wanaweza kukuimarisha kiimani au kukufanya dhaifu.
Usipinge kile unachokisikia kuhusu mwenzi wako kutoka kwamarafiki zako, yale wanayoyasema yanaweza kukusaidia katika kuboresha mahusiano yenu au katika kumfahamu vyema zaidi, usiyapuuze wala kuyapinga.
Ngazi ya nne ya mahusiano ni malengo
Malengo yako ya maisha na ndoto zako lazima ziwe na uhusiano na ndoa unayoitaka au uliyonayo.
Usifunge ndoa kwa ajili ya watoto, kwa ajili ya tendo la ndoa au kwa ajili ya kupata mtu utakayekuwa naye karibu “companionship”.
Ikiwa umefunga ndoa kwa miaka mitatu au minne na umebaki palepale kimaisha na kimtazamo basi utakuwa haujajua malengo yako au labda unaishi na usiyestahili.
Ongelea ndoto na malengo ya maisha yako ukiwa na marafiki zako. Katika ngazi ya urafiki au uchumba penda sana kuongelea ndoto zako au maono yako na huyo unayempenda ili kujua kama ndoto zenu ni halisi na je hazina migongano au tofauti kubwa?