Skip to content

UNESCO kuifufua sinema ya ‘Majestic’

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), jana imezindua mradi wa matengenezo ya jengo la sinema Majestic lililopo Vuga.

Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na mabalozi wa Japan na Saudi Arabia nchini Tanzania, ambao nchi zao zimekubali kuchangia gharama za matengenezo makubwa yanayolenga kulifanya jengo hilo kuwa kituo kikuu cha utamaduni visiwani Zanzibar.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyoshirikisha timu ya wataalamu na wadau wa Mji Mkongwe katika hoteli ya Park Hyatt, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Mohammed Mussa, alisema mradi huo unatarajiwa kubadilisha taswira ya jengo hilo.

Aidha waziri Lela alisema mradi huo utahusisha kuliwekea miundombinu na vifaa vyote vinavyohitajika kwenye shughuli za kiutamaduni na sanaa.

Alisema, matengenezo hayo yatafanywa kwa kuzingatia muongozo wa UNESCO kuhusu uhifadhi wa sura ya asili, na kuliongezea haiba ili kuvutia watalii wa nje na ndani kulitembelea kwa shughuli zao mbalimbali.

Alisema zoezi la kulifanyia matengenezo jengo hilo lilianza mwaka 2022, ambapo serikali ilitoa tangazo kuwaita wahisani mbalimbali, na kampuni ya ‘Hifadhi Zanzibar’ ilikuwa ya kwanza kujitokeza ikisema tayari imeshaanza kuzungumza na UNESCO ambayo ilikubali kulibeba jukumu hilo kwa kushirikiana na balozi za Japan na Saudi Arabia, Mamlaka ya Uhifadhi Mji Mkongwe na Idara ya Makumbusho.

Alisema baada ya uzinduzi huo wataalamu watapitia andiko la mradi kuona namna ya kuanza kazi, na kuongeza kuwa dola milioni moja za Kimarekani zinahitajika kuigharamia, na kwamba dola laki sita tayari zimepatikana.

Alizishukuru serikali za Japan na Saudi Arabia pamoja na UNESCO na wahisani wengine waliojitolea kuchangia kwa namna tafauti mradi wa kulifufua jengo hilo lenye historia kubwa nchini, Afrika Mashariki na duniani kwa jumla.

Mapema, Mwakilishi wa UNESCO nchini Tanzania, Michel Toto, aliihakikishia Serikali ya Zanzibar, kuwa shirika hilo litaendelea kuiunga mkono katika mikakati yake ya kuuhifadhi Mji Mkongwe ili kulinda historia kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe, Ali Bakari Said, alisema ni dhamira ya serikali kuyafanyia matengenezo majengo yote ya kihistoria yaliyomo mjini humo kwa kushirikiana na wahisani mbalimbali wa ndani na nje.

Alisema kutimia kwa azma hiyo, kutatoa fursa kwa vijana na wananchi wengine kuibua vuguvugu la matukio ya kitamaduni yanayofanyika kila mwaka pamoja na shughuli za kijamii na kiuchumi, ambazo huupamba mji kwa ujio wa wageni wanaoongeza pato la taifa kupitia sekta ya utalii.

Balozi wa Japani nchini Yasushi Misawa, alieleza utayari wa nchi yake kusaidia ujenzi mpya wa sinema ya Majestic, ikiamini kuwa kufanya hivyo ni sehemu ya kukuza utamaduni na maeneo ya urithi ambao ni miongoni mwa mipango mikuu ya Japan.

Yahya bin Ahmed Okeish ambaye ni Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania, alisema tayari nchi yake imetoa dola laki moja za Kimarekani katika hatua za awali za utekelezaji wa mradi huo.

Alisema Saudi Arabia inavutiwa na utajiri wa Zanzibar katika utajiri wa historia na majengo ya kale, na kwamba kupitia mradi huo, uhusiano wa nchi hiyo, Zanzibar na Tanzania kwa jumla, utaimarika maradufu.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na wadau kutoka taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi, akiwemo Balozi Mdogo wa Oman hapa Zanzibar Said Salim Al Sinawi.

Sinema ya Majestic ambayo kwanza iliitwa ‘Cinema Royal’ ilipata umaarufu tangu ilipoasisiwa mwaka 1921, na baada ya jengo la  awali kuungua moto 1951 nafasi yake ilichukuliwa na jengo hilo la sasa lililobuniwa na kujengwa na mjenzi mahiri wakati huo, Dayalji Pitamber Sachania.

Tags: