WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema serikali itaendelea kubuni mikakati ya kuimarisha sekta ya maliasili na utalii kwa kuwa ni nguzo muhimu kwa uchumi wa taifa.
Alisema hayo wakati akizindua tuzo za uhifadhi na utalii katika ukumbi wa hoteli ya Mt. Meru jijini Arusha.
Tuzo hizo zina lengo la kuchochea ushindani kati ya wadau wa sekta ya maliasili na utalii nchini.
Alisema sekta ya maliasili na utalii ni chanzo kikubwa cha mapato ya taifa kwa kuwa inahusisha shughuli nyingi za kiuchumi.
“Sekta hii peke yake inachangia asilimia 21.5 katika pato ghafi la taifa ambapo asilimia 17.2 ni utalii, asilimia 4.3 ni misitu na nyuki,” alisema.
Aidha, alisema sekta hiyo inachangia asilimia 30.9 ya mapato ya fedha za kigeni ambapo asilimia 25 yanatokana na utalii na asilimia 5.9 ni misitu na nyuki.
Katika hatua nyingine, Majaliwa alisema juhudi za dhati na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuiendeleza sekta ya maliasili na utalii yamesaidia kuongeza idadi ya watalii wa kimataifa kwa asilimia 96 kutoka watalii 922,692 mwaka 2021 hadi watalii 1,808,205 mwaka 2023.
Aliiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kuweka vigezo vya wazi na vinavyojulikana vya uteuzi na upokeaji wa tuzo.
“Vigezo hivyo, pamoja na mambo mengine viwe vinavyozingatia ubora katika uhifadhi wa mazingira, huduma za utalii, usimamizi wa hifadhi za wanyama na uendelezaji wa maeneo ya utalii,” alisema.
Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi, Dk. Pindi Chana ameipongeza serikali kwa namna inavyojitoa katika kuhakikisha sekta ya maliasili na utalii inaendelea kukuwa kwa kasi.
Aliongeza kuwa wizara hiyo ina mikakati mbalimbali ya kuimarisha uhifadhi na kuendeleza utalii ikiwemo kutumia teknolojia pamoja kuendeleza programu ya Tanzania – the Royal Tour na kuibua mazao mapya ya utalii ili kuongeza idadi ya watalii na mapato yatokanayo na shughuli za utalii.