Skip to content

Uturuki kujiunga na Afrika Kusini dhidi ya Israel

ANKARA, UTURUKI

WAZIRI wa mambo ya nje wa Uturuki, Hakan Fidan amesema kuwa nchi itajiunga na Afrika Kusini katika kesi ya kuishitaki Israel kwenye mahakama ya kimataifa.

Waziri huyo alibainisha hao alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Ankara akiwa na waziri wa mambo ya nje wa Indonesia, Retno Marchudi.

Fidan alisema Uturuki imeamua kuungana na Afrika Kusini katika kesi ya mauaji ya halaiki yanayofanywa na Israel huko Gaza.

“Tunatumai kwamba hatua hii itasaidia kuelekeza mchakato katika ICJ katika mwelekeo sahihi”, amebaini, akiongeza kuwa juhudi za Uturuki kujiunga na kesi hiyo zimekuwa zikiendelea kwa muda mrefu.

Fidan alisisitiza tena kuwa Uturuki itaendelea kuwaunga mkono watu wa Palestina katika hali zote na kufanya kazi na nchi zote rafiki na washirika ili kuamua hatua zaidi zinazowezekana na kutambua nchi zinazoweza kujiunga na ombi hili.

Mnamo mwezi Disemba mwaka jana Afrika Kusini iliwasilisha malalamiko dhidi ya Israel katika mahakama ya kimataifa ya haki, ikiishutumu kwa kufanya mauaji ya halaiki huko Gaza.

Uamuzi uliotolewa mwezi Januari mwaka huu uliiamuru Tel Aviv kukomesha vitendo vya mauaji ya halaiki na kuchukua hatua zinazohitajika kuhakikisha msaada wa kibinadamu kwa raia wa Gaza.

Vita vya Israel vilianza kuishambulia Gaza tangu Oktoba 7 mwaka jana ambapo vimesababisha karibu watu 35,000 kupoteza maisha, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Aidha katika mashambulizi hayo maelfu ya watu wamejeruhiwa na kusababisha uharibifu mkubwa na uhaba mkubwa wa mahitaji ya kimsingi.

Zaidi ya miezi sita baada ya kuanza kwa vita vya Israeli, sehemu kubwa ya Gaza iko katika magofu, na kusukuma asilimia 85 ya wakazi wa eneo hilo kutoroka mashambulio ya mara kwa mara, kulingana na Umoja wa Mataifa.