Skip to content

Vieira bosi mpya Genoa

ROME, Italia

GWIJI wa Arsenal, Patrick Vieira, ameteuliwa kuwa kocha mkuu mpya wa klabu ya ‘Serie A’ ya Genoa.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 48 anajiunga na klabu ambayo ipo katika nafasi ya 17 kwenye Ligi Kuu ya Italia, pointi moja juu ya eneo la kushushwa daraja.

Meneja huyo wa zamani wa Crystal Palace, ambaye aliondoka RC Strasbourg mwezi Julai, anarithi mikoba ya mshambuliaji wa zamani wa Italia, Alberto Gilardino, ambaye amekuwa kocha tangu Disemba 2022.

Chini ya mshindi wa Kombe la Dunia 2006, Gilardino, Genoa, ilikuwa imeshinda mechi mbili kati ya 12 za ligi msimu huu na wakatupwa nje ya Coppa Italia na Sampdoria kwa mikwaju ya penalti.

Uteuzi huo unamkutanisha Vieira na Mario Balotelli, ambaye alisajiliwa na Genoa mwezi uliopita.

Vieira alimnoa mchezaji mwenzake wa zamani wa Manchester City na Inter Milan katika klabu ya Ligue 1 ya Nice msimu wa 2018-19.

Balotelli tangu wakati huo amesema ilikuwa ni kutoelewana na Vieira kuhusu mbinu ambazo zilimfanya aondoke katika klabu hiyo mwaka 2019.

Wakati wa uchezaji wake, Vieira alishinda mataji matatu ya Ligi Kuu ya England  na manne ya Kombe la FA akiwa Arsenal, na vile vile mataji  akiwa na AC Milan, Inter Milan na Manchester City.

Pia aliisaidia Ufaransa kushinda Kombe la Dunia la 1998 na Ubingwa wa Ulaya 2000.

Vieira alistaafu mnamo 2011 na kuwa meneja wa New York City mnamo 2016.

Kiungo huyo wa zamani alirejea Ulaya na Nice na kuwaongoza kumaliza katika nafasi ya saba kwenye ‘Ligue 1’ katika msimu wake wa kwanza, lakini, alitimuliwa Disemba 2020.

Vieira alikua meneja wa Palace mnamo 2021 na kuiongoza Eagles hadi nusu fainali ya Kombe la FA.

Alitimuliwa 2023 baada ya kucheza mechi 12 bila ya kushinda, kabla ya kujiunga na Strasbourg kama uteuzi wao wa kwanza baada ya kunyakuliwa na kampuni ya BlueCo, ambayo pia inaimiliki Chelsea.(Sky Sports).