Skip to content

Wafanyabiashara, taasisi kushiriki maonesho ya  11 ya biashara

  • Zanzibar

NA HUSNA SHEHA

WAZIRI wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Omar Said Shaaban, ameeleza kuwa maonesho ya 11 ya biashara kimataifa Zanzibar yanatarajiwa kufanyika Januari 1 – 15, mwakani na kushirikisha zaidi ya washiriki 600.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kinazini, omar alieleza kuwa kwa mwaka huu maonesho hayo yatafanyika katika viwanja vya maonesho kimataifa Nyamanzi kwa unguja na Chamanangwe kwa pemba.

Alifafanua kuwa  maonesho hayo yanayokwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 61 ya mapinduzi  ya Zanzibar, kwa Unguja yataanza  Januari 1 na kumazika januari 15 na kwa Pemba yatafanyika kati ya Januari 7 na 15, 2025 yakiwa na kauli mbiu ‘Biashara mtandao kwa maendeleo ya biashara na uwekezaji’.

Aidha waziri Shaaban alisema kuwa maonesho hayo  ni miongoni mwa majukumu ya wizara iliyojiwekea kwa lengo la kuwatafutia masoko wafanyabiashara wadogo na wakubwa.

“Maonesho hayo yanatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki wapatao 500 kwa upande wa Unguja na 100 kwa Pemba, ambao tunatarajia watatoka ndani na nje ya Zanzibar”, alisema Omar. 

Alisema mbali ya wafanyabiashara wadogo wadogo, wa kati na wakubwa, taasisi za serikali na binafsi zinatarajiwa kushiriki na kuonesha bidhaa au huduma wanazozitoa.

Alisema kwa kawaida maonesho hayo huenda sambambana matukio tofauti yakiwemo makongamano ya biashara, mikutano ya ana kwa ana baina ya wafanyabiashara.

Aidha Omar alitaja mafanikio ya yaliyopatikana katika maonesho yaliyopita ambayo kwa mara ya kwanza yaliofanyika katika viwanja vya Nyamanzi kuwa ni kuwa na ongezeko la washiki kama waoneshaji na watu waliotembelea maonesho hayo.

“Licha ya changamoto mbali mbali, tulifanikisha maonesho ya 10 ambayo yalihudhuriwa na washiriki 376 ambapo kati ya hao washiriki 240 walitoka Zanzibar, 126 Tanzania bara  na 10 nje ya Tanzania kutoka nchi za Uganda (4), Burundi(2) huku nci za Zambia, Misri na Rwanda zikitoa mshiriki mmoja mmoja.

“Kulingana na takwimu zilizokusanywa wakati wa maonesho ya mwaka jana, makadirio ya mauzo ya papo kwa papo yalifikia shilingi bilioni 1.11 ambayo yalipungua kidogo kulinganisha na maonesho ya tisa ambapo mauzo yalikuwa ni shilingi  bilioni 1.66 ambayo yalifanyika katika kipindi chote cha maonesho”, alisema WazirI Omar.

Aidha aliviomba vyombo vya habari kuyatangaza maonesho hayo ili kukuza sekta ya biashara nchini na kupelekea kukuza uchumi na ni fursa ya kuyafikia masoko kwa wafanyabiashara  na wazalishaji nchini.