Skip to content

Wakulima wa mwani Kajengwa wakabidhiwa vifaa 

NA MWANAJUMA MMANGA

WIZARA ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi imekabidhi vifaa kwa ajili ya ukulima wa mwani katika shehia ya Kajengwa Makunduchi vilivyogharimu shillingi million thelathini. 

Waziri wa Wizara hiyo, Shabani Ali Othman, aliyasema hayo mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo kwa vikundi 17 vyenye wakulima 466 Huko Makunduchi Wilaya ya Kusini Unguja.

Alisema mwani umekuwa ukichangia pato la taifa kwa asilimia kubwa, hivyo kuwepo kwa vifaa vitakavosidia ukulima huo utawawezesha wakulima kufanya kazi hiyo kwa ufanisi.

Akizungumzia kuhusiana na suala la ujenzi kiwanda kwa ajili ya mwani alisema wizara itasimamia ujenzi huo kwani eneo lipo la kujenga kiwanda hicho makunduchi.

Aidha, alisema kuwa vifaa hivyo ni kutekeleza ahadi aliyoitoa kwa wakulima hao wakati akikabidhi boti ya uvuvi huku akiwataka vijana kuchangamkia fursa hiyo ili waweze kujiajiri na kuajirika. 

Alisema iwapo vijana hao wakijiajiri wenyewe watapunguza tatizo la ajira na kuachana kusubiri ajira serikalini.

“Niwaombe sana wakulima wenzangu kuhakikisha vifaa walivyopatiwa kuvifanyia kazi kama vile ilivyokusudiwa na kuvitunza ili hapo baadae vije kuzalisha na kuleta malengo.”alisema. 

Nae, Katibu wa mwani shehia ya Kajengwa, Fatma Pea Makame, akisoma risala katika ghafla hiyo, alisema wanathamini juhudi za serikali katika kuimarisha ukulima wa mwani nchini pamoja na kuiomba serikali kuwaekea bei elekezi ya mwani kwani bei iliyopo haikidhi kulingana na kazi wanayoifanya.

Mwakilishi wa Jimbo la Makunduchi, Haroun Ali Suleiman, ambae ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Katiba Sheria na Utawala  bora, amewataka wakulima kuunga mkono jitihada za serikali huku akiahidi kuendelea kushirikiana na wakulima hao.

Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Uvuvi na Mazao ya Baharini DK. Salum Soud Ahmed, alisema mwani umekuwa ukitoa fursa za kujikwamua na hali ngumu za maisha hasa kwa wanawake hivyo amesema wizara itaendelea kuwasimamia wakulima hao.

Wakati huo huo, Mwakilishi wa jimbo hilo, Haroun Ali Suleiman, alishiriki katika ghafla ya kuvunja vikoba vya wakina mama wa vikundi mbalimbali huko Makunduchi. 

Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na kamba kwa ajili ya ukulima wa  mwani katika vikundi 17, vyenye jumla ya wakulima 466 ambavyo vimegharimu shillingi millioni 30.