Skip to content

Walimu wakuu, wasaidizi waongezewa posho, 3000 waajiriwa

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, imesema imeajiri zaidi ya walimu 3000 katika maeneo tofauti ambao watakwenda kupunguza idadi ya vipindi kwa walimu wakuu.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Ali Abdulgulam Hussein alieleza hayo katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani wakati akijibu suali la nyongeza la Mwakilishi wa Jimbo la Mtambwe Dk. Mohammed Ali Suleiman.

Mwakilishi huyo alisema mpango wa serikali kuwapunguzia kazi walimu wakuu hasa kuwaondosha katika ufundishaji kwani wengi wana vipindi na wanashindwa kufundisha kutokana na mzigo mkubwa waliokuwa nao.

Alisema lengo la kuajiri walimu ni mpango wa serikali kuhakikisha walimu hao wanapunguziwa mzigo wa vipindi hasa walimu wakuu.

Naibu Gulam alisema mpango mwengine ni kuboresha miundombinu ambayo itapunguza idadi ya wanafunzi katika madarasa na kupungua kwa vipindi huku mazingira ya kujifunza na kufundishia yatakuwa mazuri.

Akizungumzia posho za walimu wakuu na wasaidizi walimu wakuu alisema wizara katika mpango mpya wanaokuja nao inakwenda kuongeza posho za walimu wakuu na walimu wakuu wasaidizi.

Alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa hamasa kubwa na kuielekeza Wizara kuongeza posho za walimu hao.

“Wakati tunapitisha bajeti nilieleza wazi kuanzia mwezi Juni maposho haya yataanza kutoka la shilingi 150,000 kwa walimu wakuu kutoka shilingi 35,000 waliokuwa wakipewa awali na kwa walimu wasaidizi kutoka 35,000 mpaka 130,000.

Naye Mwakilishi wa Jimbo la Malindi, Mohammed Ahmada Salum, alitaka kujua zimebaki siku 13 kabla ya ufungaji wa hisabu za serikali kusiwe na malipo mengine yoyote hivyo siku hizo wataweza kulipa posho na kwa kuwa umeanza Mei mpaka Juni ni kiasi gani cha fedha kitalipwa kwa walimu hao.

Alisema posho hilo walimu walikuwa walipwe tokea mwezi Juni lakini kutokana na matatizo tofauti ikiwemo ucheleweshaji wa uhakiki wa walimu na wanaendelea nao lakini taratibu zote zimekamilika na hivi sasa taratibu utaratibu katika system za mishahara majina hayo yameshapelekwa.

Naye Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini, Machano Othman Said, alitaka kujua malipo ya posho hizo yataanza kuanzia Julai mwaka huu wanaomalizia au Januari.

Naibu Gulam alisema ni kweli utaratibu huo ulikuwa uanze mapema lakini tararibu za ndani nyingi zilikuwa hazijakamilika ikiwemo kuwepo kwa idadi kubwa ya walimu wakuu ambao walikuwa wakikaimu nafasi na bado hawajathibitishwa na wengine ilikuwa vielelezo vya mchakato wa kupatikana ualimu haujakaa vizuri.

“Taratibu hizi zilichukua muda kukamilisha na kwa sasa taratibu hizi zimekamilika na mwezi Juni utaratibu huo rasmi unakwenda kuanza ikishindikana mwezi Juni na kufika mwezi Julai hawajalipwa area zao zitaanza kuanzia mwezi Juni na kwa barua tuliyoipata Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango tayari fedha hizi zitaanza kulipwa mwezi wa Juni na hakutakuwa na malipo ambayo yataanza miezi ya nyuma ikitokea hazijaingia malimbikizo yao watalipwa kuanzia mwezi Juni.

Akijibu suali la msingi la Mwakilishi wa Jimbo la Mtambwe, Dk. Mohammed Ali Suleiman, aliyetaka kujua walimu wakuu na wasaidizi wao kiasi cha posho wanachotakiwa kupewa kwa mwezi.

Alisema kiwango cha posho za walimu wakuu ni shilingi 150,000 na wasaidizi walimu wakuu ni shilingi 130,000 kiwango ambacho kimeainishwa kwa barua nambari CCB.149/550/04/39 ya Januari 13 mwaka 2024 kutoka ORKSUUB.

Alisema hadi sasa posho hilo halijaanza kutolewa kutokana na ORKSUUB kutaka kupewa uthibitisho wa bajeti kutoka Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango.

“Wizara imeendelea kufuatilia kwa karibu suala hili na tayari imepokea barua yenye kumbkumbu Nalbari CAC. 20/450/01/43/46 kutoka Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango inayoelezea kulipwa kwa posho hiyo katika robo ya nne ya mwaka 2024/2025 kuanzia Mei 2025.

Hata hivyo, alisema ni matarajio ya wizara kuwa posho hilo litaanza kulipwa rasmi katika robo hii ya nne ya mwaka 2024/2025.

Akizungumzia tathmini inayoonesha walimu wenye cheo ambao wanastahiki kupata posho hiyo kwa skuli za msingi na sekondari alisema jumla ya walimu wakuu 157 wakiwemo 64 Unguja na 93 kwa kisiwa cha Pemba na wasaidizi walimu wakuu 213 Unguja 96 na Pemba 117 wa skuli za sekondari wanastahili kulipwa posho hilo.

Alisema kwa upande wa skuli za msingi walimu wanaostahiki posho hilo ni walimu wakuu 309 Unguja 125 na Pemba 184 pamoja na wasaidizi walimu wakuu 397 wakiwemo wa Unguja 194 na Pemba 203.