NA MWAANDISHI WETU
TASNIA ya habari imepata jana pigo kufuatia kifo cha mwandishi wa habari mwandamizi, Nasra Nassor Suleiman, kilichotokea katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam.
Nasra ambaye alikuwa Mkufuzi katika Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) Tunguu, alifariki baada ya kuugua kwa muda mfupi, kabla ya kuwa mkufunzi chuoni hapo aliwahi kulitumia Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) na redio ya Swahiba FM.
Aidha wakati wa uhai wake, Nasra alikuwa mwanachama wa taasisi mbali mbali za kihabari ikiwemo Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC) na Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA).
Baadhi ya waandishi wa habari, wanafunzi na wadau wa habari, wameelezea kifo chake kuwa ni pigo kubwa kwa tasnia wakimuelezea marehemu kama mtu asiyependa makuu, kujikweza na alikuwa msaada kwa kila mtu aliehitaji kusaidiwa.
Mwandishi wa habari mwandamizi Salum Vuai Issa, alisema marehemu alikuwa mtu wa watu, aliesikiliza mawazo ya kila upande na aliejitolea kusaidia wengine.
Naye Dk. Saleh Yussuf Mnemo, alimtaja marehemu kuwa ni miongoni watu wakarimu na atakumbukwa kwa jinsi alivyokuwa akiwasaidia waandishi wenziwe wakati wa kutekeleza majukumu yao.
“Nilikuwa naye masomoni nchini China na ndipo nilipomfahamu kwa ukaribu zaidi kuliko wakati ambao tukifanya kazi pamoja tukiwa ZBC (Shirika la Utangazaji Zanzibar). Alikuwa mcheshi, mkarimu na anayependa watu asiyekata tama katika kujifunza”, alieleza Dk. Mnemo.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC), Abdallah Abrahman Mfaume, alimtaja marehemu kama mfano bora wa wandishi wa habari hasa wanawake kwani alikuwa hapendi uonevu wala kupindisha ukweli.
“Marehemu alikuwa msomi mzuri wa fani ya habari na alikuwa mwenye msimamo juu ya mambo anayoyaamini vitu ambavyo ni msingi mzuri kwa waandishi wa habari kwani kazi hii inahitaji uthubutu, kujiamini na kusimamia unayoyaamini”, alieleza Mfaume.
Nao Katibu Mkuu wa WAHAMAZA, Salma Said na wa ZPC, Mwinyimvua Abdi Nzukwi, walisema kifo cha Nasra kimeacha pengo kubwa katika tasnia ambalo litachukua muda mrefu kuzibika kutokana na juhudi zake za kusaidia waandishi hasa chipukizi.
“Kwangu nasra alikuwa mwenzangu, mwalimu, rafiki na kiongozi aliyekuwa tayari kuongozwa kwani mara nyingi alitoa na kupokea mawazo hata kwa watu ambao amewazidi kiumri au kielimu”, alieleza Salma.
Akizungumza kwa niaba ya Chuo Kikuu cha Zanzibar, Dk. Suleiman Seif, alisema chuo kimepoteza kiungo muhimu akimuelezea marehemu kama mchapa kazi aliejitolea kusaidia kila mtu.
Naye kaka wa marehemu, Yahya Nassor Suleiman, alisema kifo cha Nasra kilisababishwa na msongo wa mawazo kufuatia kifo cha ghafla cha mwanafunzi mwenzake aliyekuwa akisoma nae shahada ya uzamivu (PhD) nchini Malaysia.
“Kifo chake kilisababishwa na msongo wa mawazo kutokana na kifo cha mwanafunzi mwenzake ambae alikuwa kama kaka kwake, hivyo wakati yuko chooni anakoga akadondoka na kujigonga kichwani akazimia”, alisema Yahya.
Alisema awali alitibiwa katika hospitali ya Mnazimmoja zanzibar kabla ya kuhamishiwa hospitali ya Muhimbili ambapo alikaa kwa siku 1O na baadae akazinduka na kutoa matumaini kwa wanaomuuguza.
“Lakini jana alipata kama pumu, nikawauliza madaktari wakasema kwa sababu anakula kwa mpira inatokea wakati mwengine chakula kinapopotea kikiingia kwenye mapafu inakuwa shida, hali yake ikawa haitabiriki na leo (jana) kama saa tatu asubuhi alifariki”, aliongeza Yahya.
Taarifa za kifo cha Nasra zilianza kuzagaa katika majukwaa maalum ya waandishi wa Habari Zanzibar Majira ya asubuhi na kisha taarifa kueleza kuwa maziko ya mwanahabari huyo aliyezikwa katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es salam.