NA FAUZIA MUSSA
MKURUGENZI wa shirikika linalojihusisha na mabadiliko ya tabianchi ‘CAN TANZANIA’, Dk. Suxbert Mwanga, amewataka waandishi wa habari kuandika habari zinazohusiana na mabadiliko ya tabia nchi ili kuisaidia jamii kufahamu athari na njia za kukabiliana nayo.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wanahabari hao, alieleza kuwa mabadiliko ya tabianchi yanachangiwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia yanayokwenda sambamba na maendeleo ya watu.
Alisema ipo haja ya jamii kuelimishwa juu ya athari na madhara ya mabadiliko ya tabianchi na namna ya kuidhibiti hali hiyo kwa kuacha kuendelea kutumia na kufanya mambo yanayochangia kuepusha madhara ikiwa ni pamoja na kutumia nishati zisizozochafua mazingira.
“Tanzania kama sehemu ya dunia nayo itaendelea kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi endapo haitakua na mikakati madhubuti ya kukabiliana na hali iliyopo pamoja na kuitekeleza ipasavyo”, alieleza Dk. Mwanga.
Aliwashauri viongozi wa kisaisa kuiingiza mikakati hiyo katika ilani za vyama vyao ili itekelezeke kwa haraka huku akisema hatua hiyo itachochea kupunguza shughuli za kibinadamu zinazochochea mabadiliko hasi ya hali ya hewa, uchomaji wa nishati ya mafuta, matumizi ya makaa ya mawe, mafuta na gesi chafu.
Alifafanua kuwa kwa kutambua uwezo wa wanahabari katika kuifika jamii, shirika hilo limeamua kuandaa mafunzo hayo ili kuwajengea uelewa utakaowasaidia kutekeleza vyema majukumu yao ipasavyo jambo alilolitaja kuwa litasaidia uandaaji wa mipango ya kuhakikisha athari za mabadiliko ya tabianchi haziendelei.
Kwa upande wake Mtendaji wa taasisi hiyo, Mkombozi James Mbekenga, alieleza kuwa mabadiliko ya tabianchi ni suala mtambuka ambalo haliishi kumwathiri binaadamu pekee bali linagusa mazingira, uchumi na kuathiri mipango ya maendeleo ya nchi na eneo husika.
Alisema uzoefu unaonesha kuwa hali hiyo inamuathiri kila mtu lakini kundi la wavuvi, wakulima, wafugaji, wanawake na watoto ndio huathiriwa zaidi hivyo aliwaomba waandishi kuyafikia zaidi makundi hayo katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Shukeni walipo wananchi wa chini hasa maeneo ya vijijini mkaangalie na kufanya tafiti zinazoonesha maeneo yaliyoathariwa na mabadiliko ya tabianchi na matokeo yake yatatusaidia sisi na dunia kwa ujumla kujua Afrika iko katika hali gani”, alisisitiza Mkombozi.
Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo, ofisa kutoka taasisi ya Nishati Jadidifu Tanzania (TAREA), Mathew Matimbwa, aliwashauri waandishi kuelezea umuhimu wa kutumia nishati zinazorudishika kwa haraka bila kuchafua mazingira ikiwa ni njia moja wapo ya kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi, pamoja na kupunguza gharama za matumizi ya nishati.
Aliizitaja baadhi ya nishati hizo kuwa ni pamoja na umeme, nguvu ya upepo, maanguko ya maji na ongamo taka.
Mmoja ya waandishi wanaoshiriki mafunzo hayo, John Edward Kabambara, alisema yatawasaidia kufanya kazi zao kwa weledi na ufanisi huku kuhadi kuyafanyia kazi ili malengo yaweze kufikiwa.
Aidha waliziomba taasisi na mashirika husika kuwapa mashirikiano wakati wa kukusanya taarifa zinazohusiana na mabadiliko ya Tabia nchi ili kuzifikisha ndani ya jamii kwa wakati na kwa usahihi.
Mafunzo hayo yaliyowakutanisha waandishi wa habari wa mikoa ya Tanzania bara na zanzibar mada mbali mbali ziliwasilshwa na wakufunzi kutoka mamlaka ya hali ya hewa tanzania (TMA), TAREA na chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM).