NA ROBERT HOKORORO
WATAFITI kutoka Nchi zinazozunguka Ziwa Tanganyika wametakiwa kushirikiana katika kufanya utafiti, ili kubaini chanzo cha kuongezeka kwa kina cha maji cha ziwa hilo ili kudhibiti hali hiyo inayoathiri mazingira.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bonde la Ziwa Tanganyika (LTA) Sylvain Mukanga wakati akifungua Mkutano wa Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Ziwa Tanganyika ngazi ya wataalamu wa kujadili kuongezeka kwa kina cha maji ya Ziwa Tanganyika, unaofanyika jijini Dar es Salaam.
Amesisitiza kuwa mkutano huo huo unaowahusisha wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara za kisekta na wataalamu wengine kutoka Zambia, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kilete suluhu ya changamoto ya kujaa kwa maji katika ziwa hilo.
Mukanga amesema kuwa kina cha Ziwa Tanganyika kimekuwa kikiongezeka kila mwaka kutokana na shughuli za kibinadamu zisizo endelevu zikiwemo ukataji wa miti na uvuvi haramu hivyo ni wakati sasa wa kujadili namna bora ya kupunguza changamoto hiyo.
Pia, ameeleza kuwa kuongezeka kwa kina cha maji ya ziwa hilo huchangia kwa kiasi kikubwa katika uharibifu wa mazingira ambao husababisha mafuriko na hivyo kuathiri shughuli za wananchi wanaozunguka eneo la bonde la ziwa.
“Tangu mwaka 2019, mvua kubwa zilizonyesha katika kipindi hicho zimesababisha mafuriko, mmomonyoko wa ardhi na upepo mkubwa na hivyo kusababisha kina cha maji cha Ziwa Tanganyika kuongezeka, hii ni hatari kwani mafuriko hayo yameleta athari katika miundombinu iliyopo katika maeneo mbalimbali yanayozunguka ziwa,” amefafanua.
Naye Jamson Bakuza kutoka Wizara ya Maji ametaja athari zilizotokana na kujaa kwa maji ya Ziwa Tanganyika kuwa ni kuharibika kwa miundombinu kuharibika kwa nyumba takriban 50 eneo la Katubuka pamoja na magonjwa hatari ya mlipuko kama vile.
Mkutano huo ni maandalizi ya Mkutano utakaowahusisha mawaziri kutoka nchi nne zinazozunguka Ziwa Tanganyika unaotarajiwa kufanyika Oktoba 04, 2024 jijini Dar es Salaam ambapo Tanzania itawakilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ambao nao utatanguliwa na Mkutano wa Kamati ya Ushauri wa LTA.