Skip to content

‘Watu wenye ulemavu kuendelea kupewa kipaumbele’

NA FAUZIA MUSSA

WAZIRI wa nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Harusi Said Suleiman,  amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa kipaumbele kwa watu wenye ulemavu ili kushiriki katika harakati mbali mbali za maendeleo nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri huyo, katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya  viziwi duniani yaliyofanyika Jongowe wilaya ndogo Tumbatu, Katibu Mtendaji Baraza la Taifa la watu wenye ulemavu Zanzibar, Mhandisi Ussi Khamis Debe, alisema hatua hiyo itasaidia katika  kuhakikisha  ushiriki na ushirikishwaji wa watu hao  kwenye  nyanja mbalimbali za  kimaendeleo unaonekana.

Alisema ili kufanikisha adhma hiyo ni lazima  jamii ijifunze  lugha ya alama ili  kurahisisha mawasiliano kwa kundi  hilo hali itakayosaidia kurahisisha  ushiriki na ushikishwaji wao katika harakati za maendeleo ya taifa.

“Watu viziwi wana haki ya kikatiba kama  watu wengine katika nyanza zote za kimaendeleo nchini ni vyema wakathaminiwa na kupewa kipaumbele katika familia na  ngazi zote”, lisema mhandisi Debe.

Wakati huo huo alikitaka chama cha viziwi  kuanzisha  vikundi vya ujasiriamali ili  kupata fursa ya  mikopo inayotolewa kwaajili yao (four four two) na kujikwamua kiuchumi.

“Asilimia mbili ya fedha zinazo kusanywa na manispaa ni kwaajili yenu andaeni vikundi na mufuate  taratibu za kupata fedha hizo kwa misingi ya kujikwamua kimaisha”, alieleza Debe.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Zanzibar (CHAVIZA) Asha Ali Haji na Katibu wa chama hicho, Abdalla Alawi Abdalla, alisema viziwi wanakabiliwa na changamoto ya mawasiliano ndani ya jamii kutokana na kutokujua lugha ya alama kuweza kuwasiliana nao.

Walisema kundi hilo linakosa  walimu wa kutosha Maskulini, vyuo vikuu na hata madrasa hali inayowafanya kutoshiriki ipasavyo katika kutafuta elimu na kuziomba serikali kulipa umuhimu suala la  lugha ya alama kwa jamii ili kupata haki zao kama wanavyopata wengine

Walieleza kuwa  kukosekana kwa wakalimani katika baadhi ya sehemu za kutolea huduma za jamii kama hospital, sehemu za biashara katika vyombo vya usafiri kunawakosesha kupata taarifa muhimu ipasavyo zinazotolewa katika maeneo hayo.

Mbali na hayo  aliiomba serikali na wadau wa maendeleo kuwasaidia kupata jengo la ofisi la chama hicho ili kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Katibu Tawala wa Wilaya ndogo Tumbatu, Khatib Habibu Ali, aliwapongeza wanachama wa CHAVIZA kwa kufanya hafla hiyo kijijini Tumbatu jambo ambalo alilitaja kuleta mwamko wa jamii ya kijiji hicho kuona umuhimu wa kundi hilo na kuleta mabadiliko.

Aidha Katibu huyo aliihimiza jamii kutowaficha watoto wenye ulemavu kwani wanapaswa kupata haki za msingi kama wanavyopata watoto wengine.

Mapema Katibu Tawala  alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Husein Ali Mwinyi kwa jitihada za maendeleo zinazoendelea nchini pamoja nakuwapa kipaumbele watu wenye ulemavu katika nyanza zote za maendeleo hayo.

Wiki ya Viziwi Duniani huadhimishwa  kila ifikapo wiki ya mwisho ya  Septemba,  kwa lengo la kuiunganisha jamii ya  viziwi na kuwa na sauti moja  ya kutetea haki zao wote, ambapo kauli mbiu yam waka huu  ni ‘Ungana kutetea haki za  lugha ya alama’.