Skip to content

Waziri Pembe asisitiza mashirikiano kukomesha udhalilishaji 

  • Zanzibar

WAZIRI wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Riziki Pembe Juma, ameeleza kuwa maadhimisho ya siku 16 za kupinga udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto yalilenga kutathimini juhudi zinazochukuliwa kupambana na vitendo hivyo.

Waziri huyo alieleza hayo jana wakati wa kilele cha siku 16 za uanaharakati kupinga vitendo vya  udhalilishaji zilizofanyika katuka Kiwanja cha kufurahishia watoto Tibirinzi Chake Chake, Pemba.

Alisema kuwa ni jukumu la kila mmoja kutafakari na kuchukua juhudi za makusudi katika kuondosha tatizo hilo, ili jamii na kizazi viendelee kuishi bila athari zozote zitokanazo na vitendo hivyo.

Alisema kuwa asilimia kubwa ya watu wanaofanya vitendo hivyo ni wanaume, hivyo kila mmoja kwa nafasi ana haki ya kuiambia jamii hasa wanaume na vijana wa umri wa kati kwamba matukio hayo hayaleti tija kwa jamii.

Alieleza kuwa Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, aliunda Wizara hiyo na kufungua milango kwa wanaume na wanawake kuona kwamba nao wanapo pahala pa kuelezea changamoto zao.

Hivyo aliitaka jamii kwa ujumla kila mmoja kwa nafasi yake, kusimama kuwa mtoaji wa elimu ndani ya jamii hasa kwa watoto wenyewe kuwambia wanapoona ishara tu ya kutaka kuhujumiwa iwe na baba au mtu mwengine basi wawe na uthubutu wa kukataa bila woga.

Aidha alimuomba Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Rashid Hadid Rashid, kuwa balozi kwa wanaume wenzake na kuwaelekeza sehemu husika ya kufikisha changamoto zinazosababishwa na wanawake wao ili ziweze kutatuliwa.

Mapema Mkuu huyo wa Mkoa, alisema kuwa kutokana na kufanyika kwa vitendo hivyo siku hadi siku, kuna haja ya kuwepo kwa mashirikiano baina ya wazazi na vyombo vya ulinzi na usalama, ili akusudi iwepo nguvu kubwa yakupinga na kuondosha vitendo hivyo.

Alieleza kuwa ili kuona wanapambana vitendo vya udhalilishaji kwa wale wenye akili zao timamu ikilinganishwa na umri pale inapotokea kesi hizo basi isiangaliwe upande mmoja wa kiume  bali ziangaliwe pande zote mbili.

Alifahamisha kuwa kwa mtoto wa kike mwenye miaka 18 akiwa na akili timamu huondoka nyumbani kwao kwenda kwenye mazingira anayoyafahamu yeye wakiwa na makubaliano na mwanamme, halafu ikitokea kesi anayetiwa hatiani ni mtoto wa kiume pekee,jambo ambalo si jema.

Hivyo alimuomba Waziri suala hilo kuliangalia kwa macho mawili na kulizingatia ili kuona wanapambana na udhalilishaji kwa mwanamke na mwanamme.

Alieleza tatizo jengine ambalo lipo katika masuala ya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia ni kuhakikisha wale wapambanaji wa vitendo hivyo waliomo kwenye Shehia kusaidiwa kwa namna moja ama nyengine ili waone ni jinsi gani wanazidisha nguvu yakupambanana vitendo hivyo.

Akitoa salamu kwa niaba ya Waratibu wenzake,mratibu wanawake na watoto kutoka Mchangamrima Ole Pemba, Raya Said Ali, alisema kuwa katika harakati zao za kupinga vitendo hivyo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ambazo zinarejesha nyuma juhudi zao.

Alisema moja ya changamoto hizo ni pamoja na usafiri pale inapotokea kesi usiku basi wanapata changamoto kubwa hadi kufika kwenye tukio, hivyo aliiomba wizara husika kuwatatulia changamoto hiyo kwa namna yoyote inayowezekana ili waweze kufanya kazi zao kwa wakati.