Skip to content

WEMA kuajiri walimu 63 elimu mjumuisho

  • Zanzibar

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar,  inatarajia kuajiri walimu wapya 63 wenye fani ya elimu mjumuisho ili kurahisisha suala zima la utoaji wa elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo,  Abdulgulam Hussein, aliyasema hayo katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Chukwani mjini Unguja wakati  akijibu suala la Mwakilishi wa Nafasi za Wanawake, Mwanajuma Kassim Makame, alietaka kujua hatua ambazo serikali imelenga kutatua changamoto za elimu mjumuisho katika skuli. 

Gulamu alisema Wizara inatambua changamoto mbalimbali katika elimu mjumuisho ikiwemo vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na uhaba wa waalimu.

Alisema kwa upande wa uhaba wa vifaa tayari serikali imenunua vifaa mbalimbali ikiwemo virikodi sauti 30, viti vya magurudumu 48, mashine za nukta nundu 40, glasi za kukuza vinasaba na miwani 2324.

Vifaa vyengine ambavyo vimenunuliwa alisema  ni pamoja na Laptops saba, orbit readers mbili, shimeshikio 200, baskeli za maringi matatu sita na fimbo nyeupe 65.

 Aidha alisema pamoja na ununuzi wa vifaa hivyo serikali, imevifanyia matengenezo vifaa ambavyo vimeharibika kama vile mashine braille. 

Kwa upande wa uhaba wa waalimu alisema, serikali inaendelea na hatua za kuwajengea uwezo walimu kwa kuwapatia mafunzo ya muda mrefu na mfupi.

 Alisema jumla ya waalimu wa skuli 51 kati yao 34 Unguja na 17 walipatiwa mafunzo kuhusu utawala mpya na namna ya kuwaongoza wanafunzi katika kuvitumia vifaa hivyo.

Sambamba na hayo alisema sababu zinazopelekea upungufu wa vifaa vya kufundishia ni ongezeko la wanafunzi wenye mahitaji maalumu kubadilika kwa mtaala ambao umependekeza matumizi ya vifaa vipya kwa wanafunzi na uchakavu wa vifaa vinavyotumika unaosababishwa na mazingira ya kuhifadhia pamoja na ukosefu wa vupuri.