Skip to content

Wizara yatahadharisha ulaji dawa kabla ya kupima afya

NA THUREYA GHALIB ,PEMBA

OFISA Mdhamini Wizara ya Afya Pemba, Khamis Bilali Ali, amewataka wananchi kutotumia dawa kabla ya kuangalia afya zao, ili kuondosha usugu wa maradhi waliyonayo.

Wito huo, aliutoa wakati akizungumza na wadau wa afya juu ya

uhamasishaji wa kumaliza maradhi ya malaria nchini huko ukumbi wa TC Michaikaini Wilaya ya Chake Chake  Mkoa wa Kusini Pemba.

Mdhamini huyo, alisema kuna kawaida ya wananchi kutumia dawa bila kujua ugonjwa gani walionao ,ikiwemo malaria hivyo kuna ugumu wa maradhi kutosikia dawa .

“Ni kawaida hii sasa imekuwa kawa mazowea watu kutumia dawa kiholela bila ushauri wa daktari ,jambo ambalo hupelekea kuhatarisha afya zao na maisha kwa ujumla “, alisema.

Alifahamisha kuwa vifaa vya kuchunguzia maradhi vipo vya kutosha kwa wilaya zote, ili kufahamu hali ya ugonjwa wa malaria na mengineyo yakoje .

Alisema afya ndio kitu pekee kinachomuwezesha mwanaadamu kufanya shughuli zake kwa kujiletea tija yeye mwenyewe na Taifa kwa ujumla ,hivyo alishauri wananchi kuchunguza afya zao.

Mapema Mkuu wa Kitengo cha Uhamasishaji Malaria Pemba, Yussuf Juma  Ali, alifahamisha kuwa kitengo cha uhamasishaji kinafanya jitihada za kuhakikisha malengo ya kumaliza malaria ifikipo 2028 yanafikiwa.

“Sasa hivi tunachotaka mtu yoyote asitumie dawa kabla ya kuangalia afya zao  ,na dawa zetu za malaria zipo akigundulika mgonjwa atatibiwa nakuondokana na ugonjwa huo”, alifafanua.

Aidha  aliwataka wananchi kutumia vyandaruwa walivyopatiwa ili kuweza kujikinga na maradhi hayo hatari ya malaria.

Akiwasilisha mada ya uhamasishaji katika mkutano huo afisa

uhamasishaji kutoka kiteno cha malaria Pemba, Zaina Almas  Kombo alisema amekuwa akifanya ufuatiliaji wa matumizi ya vyadharua vyenye dawa kila baada ya robo mwaka. Hata hivyo , alisema kitengo chao kimekuwa  kikikagua utoaji wa vyandarua kwa mama wajawazito na watoto katika vituo vya afya ili kuona ni kwa namna gani wanamaliza maradhi hayo.