NA ASYA HASSAN
ZANZIBAR inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa teknolojia 2025 (Zanzibar Tech Summit 2025), unaotarajiwa kufanyika kuanzia Julai 3 – 5, mwaka huu.
Kongamano hili la kipekee limeandaliwa kwa lengo la kuwaleta pamoja wadau wa teknolojia, biashara na ubunifu kutoka ndani na nje ili kujadili na kuimarisha matumizi ya teknolojia katika sekta mbalimbali za biashara na maendeleo.
Muandaaji wa kongamano hilo, Dk. Augustine Rutasingwa kutoka Zanziholics Digital Agency, akizungumza na vyombo vya Habari, alisema mkutano huu utakuwa na kaulimbiu isemayo; ‘Kuwekeza Katika Ubunifu ili Kujenga Afrika ya baadae’.
Alifafanua kuwa kongamano hilo litatumika kama jukwaa la kubadilishana mawazo, kuonesha teknolojia mpya na kujifunza mbinu bora za kutumia teknolojia, kuboresha biashara na maisha ya kila siku.
“Washiriki watapata nafasi ya kujifunza kutoka kwa wataalamu wa teknolojia, kushiriki miradi bunifu na kuchunguza mbinu mpya za kidijitali zinazoweza kusaidia biashara zao,” alisema Dk. Rutasingwa.
Aidha alieleza kuwa mkutano huu sio tu ni fursa ya kujifunza bali ni njia ya kutafuta suluhisho kwa changamoto zinazoikabili biashara na jamii kupitia ubunifu wa kiteknolojia.
Hivyo aliwataka wafanyabiashara na wabunifu kuhamasika kushiriki kikamilifu ili kupata maarifa mapya na kubadilishana uzoefu, huku wakilenga kujenga Afrika yenye mwelekeo wa kidijitali na uvumbuzi.
Alifahamisha kuwa jukwaa hilo pamoja na wafanyabiashara kupata fursa na mbinu mpya za kujifunza mambo mbalimbali kwa ajili ya maendeleo yao na taifa kwa ujumla lakini hatua hiyo pia itasaidia wageni watakaokuja kutoka nchi mbalimbali wataweza kuitangaza Zanzibar lakini pia kuongeza mapato ya nchi.
Kwa mujibu wa muandaaji mwenza kutoka Rock Yacht, Daniel Voltaire Meiller, alisema mitandao ya kidijitali inapaswa kutumiwa kwa njia sahihi ili kusaidia ukuaji wa biashara.
Naye mkurugenzi wa Zanzibar Startup Association (ZSA), Ikram Ramadhan Soraga alisisitiza mchango wa teknolojia katika kuchochea maendeleo ya biashara na uchumi na kueleza kuwa mbali na mijadala, siku ya mwisho ya kongamano hilo washiriki kutembelea vivutio vya utalii vya Zanzibar.
Zanzibar Tech Summit 2025 limeandaliwa kwa ushirikiano baina ya Zanziholics Digital Agency, Rock Yacht, Zanzibar Startup Association (ZSA) na wadau wengine unatarajiwa kuwa moja ya mikutano muhimu ya teknolojia barani Afrika unaoleta pamoja wadau wa sekta hiyo kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya kidijitali na mustakabali wa Afrika kupitia ubunifu.