Skip to content

Zanzibar kuwa mwenyeji mkutano sekta ya anga

ZANZIBAR inatarajiwa kuwa mwenyeji katika mkutano mkuu wa sekta ya anga barani Afrika ambao utavishirikisha viwanja vya ndege 20 na mashirika ya ndege 48 duniani.

Akizungumza na wadau mbali mbali wa sekta ya anga na utalii Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Seif Abdallah Juma, alieleza kuwa mkutano huo unaoitwa AVIADEV utahusisha washirika wa viwanja vya ndege duniani zaidi ya 500.

Alisema wageni wengine watakaoshiriki ni pamoja na wawekezaji kutoka sekta ya utalii, anga na wajenzi wa ndege kutoka nchi mbali mbali duniani.

“Malengo ya mkutano huu ni kuwaleta wadau mbali mbali Afrika na nchi nyengine duniani ili waweze kutumia fursa ya kuanzisha safari kutoka sehemu tofauti duniani”, alisema.

Hata hivyo, alisema dhamira nyengine ya mkutano huo ni kuunganisha sekta ya anga na utalii ili nchi inufaike na kuongeza pato la taifa.

Alifahamisha kwa upande wa Zanzibar inatarajiwa kupata manufaa makubwa, ambapo kwa sasa yapo mashirika ya ndege tayari yameonesha nia ya kuanza kufanya safari zao kuanzia Juni mwaka huu.

“Zanzibar ina nafasi nzuri kidunia pia ina vivutio vingi vya utalii na tunatarajia kupata ujio mkubwa wa watalii baada ya mkutano huo ambao utafanyika Juni 11 hadi 13 katika ukumbi wa Golden Tulip”, alisema.

Akizungumzia kuhusu mpango wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Seif alisema kwa kushirikiana na Serikali imejipanga vyema na inaendelea kuimarisha miundombinu pamoja na kukamilisha mradi wa ujenzi wa Terminal II ambao unachukua abiria zaidi ya milioni 1.4.

Nae mdau wa sekta ya anga, Bethed Areas, alisema wamepokea vizuri taarifa za mkutano huo ambao utatoa fursa kwa uchumi wa Zanzibar sambamba na kuonesha mambo mazuri ambayo yametekelezwa na serikali kwenye Ssekta ya utalii.

Alisema Zanzibar ina kiwanja kizuri cha ndege cha kisasa na pengine ni bora kuliko viwanja vyengine vya Afrika Mashariki, hivyo itahakikisha wadau wa sekta hiyo wanawajibika vyema kutangaza vivutio vilivyomo nchini.

“Kwa kutumia jukwaa hili ni nafasi yetu sasa kuyatangaza na kuonesha yale mazuri yaliyomo katika visiwa vyetu”, alisema.

Aidha alisema anaamini kuwa Zanzibar ina fursa nyingi sana na bado ina nafasi ya kushajihisha mashirika mengi ili kupiga hatua zaidi ya kuongeza mapato kupitia sekta ya anga.