Skip to content

Zanzibar, Oman kushirikiana kurudisha Beit El Ajaib, People’s Palace

NA AMEIR KHALID

WAZIRI wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Ramadhani Soraga, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, itashirikiana serikali ya Oman kuhakikisha majengo ya Beit al Ajaib na People’s Palace (Jumba ya wananchi) yanarudi katika uhalisi wake kwa kufanyiwa ukarabati.

Akizungumza na ujumbe kutoka nchini Oman uliongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia Fedha na Utawala, Khalid Almuslahi, soraga alieleza kuwa mbali na majengo hayo pia wataangalia majengo mengine yaliyomo ndani ya Mji Mkongwe yafanyiwe ukarabati mkubwa ili kuwa na haiba ya kuvutia.

Alisema ugeni huo ni muhimu kwa Zanzibar na wizara yake kwani kumekuwa na mashirikiano ya muda mrefu baina ya SMZ na serikali ya Oman katika mambo mengi hususani yanayohusu utalii wa urithi.

‘’Lengo la ziara hii ni kuhakikisha ushirikiano baina ya nchi mbili hizi unazidi kuwa na manufaa zaidi kwa wananchi wa nchi mbili katika mambo mbali  mbali’’, alisema Soraga.

Aidha aliushukuru ujumbe huo kwa kufika Zanzibar na serikali ya Oman kuendelea kutoa misaada yake kwa Zanzibar, ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa chachu ya kuleta maendeleo na kuiomba kuendelea kutoa misaada.

Alisema Zanzibar ina kila sababu ya kuendelea kudumisha udugu huo uliodumu kwa muda mrefu, ambapo kupitia ziara kama hizo zinaleta wananchi wake karibu.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Almuslahi, alisema Oman na Zanzibar zina ushirikiano wa muda mrefu, hivyo nchi hiyo itahakikisha miradi yote iliyopangwa kufanywa na Oman inamalizika kama ilivyopangwa.