NA FAUZIA MUSSA
TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kukagua taarifa zao wakati wa zoezi la uwekaji wazi wa daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya pili ili kuhakikisha usahihi wa taarifa zao kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa ZEC, Jaji George Joseph, alipokuwa akitembelea vituo kukagua zoezi hilo katika wilaya za Mjini na Kati Unguja na kusisitiza kuwa hatua hiyo ni hatua muhimu inayowawezesha wananchi kuthibitisha wapiga kura halali hivyo kuufanya uchaguzi kuwa huru, wa haki na wenye kuaminika.
“Tunaliweka wazi daftari la wapiga kura kabla ya uchaguzi ili kuthibitisha wapiga kura halali na kufanya uchaguzi kuwa huru na wa haki”, alisema Jaji Kazi.
Aliongeza kuwa zoezi hilo huepusha taarifa zisizo sahihi ambazo zinaweza kuleta mtafaruku wakati wa kupiga kura na kuwakumbusha wananchi kuwa zoezi hili litadumu kwa siku saba kuanzia Mei 24, 2025.
Aliongeza kuwa daftari litawekwa wazi katika vituo vyote vilivyotumika wakati wa uandikishaji Unguja na Pemba hivyo ni vyema wananchi wakahudhuria mapema ili tume ifanye maekebisho ya taarifa zilizokosewa na zisizo sahihi.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika zoezi hilo walieleza kuridhika na utaratibu huo akiwemo Asha Hamad Bakari mkazi wa Jumbi, alisema amekiuta taarifa zake zipo sahihi kama alivyozitoa wakati wa uandikishaji na hakuna changamoto yoyote aliyokutana nayo wakati wa zoezi hilo.
Naye Kombo Juma mkazi wa Kibele, aliwahimiza wananchi waliojiandikisha kujitokeza na kufanikisha zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kupata fursa ya kufanyiwa maboresho endapo kutakuwa na kasoro zozote katika taarifa zao.
Zoezi hili linaendelea katika vituo vyote vya uandikishaji Zanzibar ili kuhakikisha kila Mzanzibari aliyendikishwa kuwa mpiga kura anapata haki hiyo bila vikwazo na kushiriki katika mchakato huo wa kidemokrasia.
Soma habari zaidi
-
Helikopta yavuruga mkutano wa CCM Moshi
-
Zanzibar kuandaa mkutano wa teknolojia
-
Walimu wakuu, wasaidizi waongezewa posho, 3000 waajiriwa
-
Msiwalaze watoto wa jinsi tofauti chumba kimoja – ACP Akama
-
Askari polisi jela maisha kwa kusafirisha mirungi
-
Soraga: Mabalozi utangazeni utalii kimataifa
-
Elementor #2332
-
Sani Abacha dikteta aliyepora mamilioni ya dola Nigeria
-
Dk. Mwinyi: Tunathamini uhusiano wa dhati na China
-
Zaidi ya maofisa polisi 1000 wamekufa Kenya