Skip to content

ZFF yatangaza kufunga dirisha la usajili

NA MWAJUMA JUMA

SHIRIKSHO la Soka Zanzibar (ZFF) limetangaza kufunga dirisha la uhamisho na usajili kwa msimu wa ligi 2024/2025.

Hayo yamethibitishwa na mtendaji mkuu wa Bodi ya ligi Issa Kassim Ali, alipozungumza na mwandishi wa habari hizi huko ofisini kwake Mbuyu Mnene.

Alisema zoezi hilo lilianza Agosti 1 mwaka huu, na lilitarajiwa kufungwa Septemba 4, lakini liliongezwa siku tano ili kufidia siku ambazo mfumo ulikuwa na changamoto .

Hivyo alisema kuwa usiku wa kuamkia jana, dirisha hilo lilifungwa na kwa sasa hakuna siku nyengine za nyongeza.

“Tumekamilisha zoezi hilo na sasa hatuna siku nyengine za nyongeza na timu ambayo haijamaliza itasubiria dirisha dogo”, alisema.

Hata hivyo alisema anashukuru viongozi wa klabu walizitumia vyema siku tano za nyongeza ambazo ziliongezwa ili kutoa nafasi ya kukamilisha taratibu ambazo zilikuwa hawajazimaliza.

“Tunashukuru zoezi letu limekwenda vizuri na viongozi walijitahidi kuzitumia vyema siku hizo na kiukweli zoezi zima limekwenda vizuri”, alisema.

Hivyo aliwataka viongozi wa klabu kuhakikisha wanashiriki ligi zao kwa njia ya amani na kuacha kufanya udanganyifu.