NA MAUA ALLY
MAMLAKA ya Mapato Zanzibar (ZRA), imesema itaendelea kushirikiana na wafanyabiashara ili kuhakikisha lengo la serikali la kuanzisha mamlaka hiyo kukusanya mapato linafikiwa.
Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, Said Ali Mohammed, alieleza hayo katika ziara ya kuwatembelea walipa kodi wa Mkoa wa Magharibi Unguja ikiwa ni mwezi wa kuwashukuru na kuwapongeza walipakodi wa Zanzibar.
Alisema bila ya wafanyabiashara kushirikiana pamoja na mamlaka hiyo, haitaweza kutekeleza jukumu lake la ukusanyaji wa mapato kwa mujibu wa sheria.
Alifahamisha kuwa wafanyabiashara wana mchango mkubwa katika maendeleo kwa jamii kupitia kodi wanazolipa katika serikali jambo ambalo huleta hamasa kwa mamlaka hiyo kutambua namna ya kuwasaidia kulipa kodi anayostahili kulingana na biashara wanazofanya.
Alieleza kuwa kodi zinakusanywa kwa mujibu wa sheria na utaratibu ambazo hazihitaji mtu mmoja mmoja na pia wanafahamu kuwa biashara nyingi zinatumia mikono lakini serikali inatekeleza majukumu yake kwa kufuata sheria.
Said alibainisha kuwa kwa kulitambua hilo waliona kuwa kutokana na hali hiyo wafanyabiashara wanapofanya biashara ndani ya mwezi huo basi walipe mwezi unaofuata kwa mauzo ya mwezi huo ili kuweza kulipa kwa urahisi na mapema.
Akizungumzia mwezi wa shukrani alisema mamlaka hiyo umeutenga mwezi wa Disemba kuwashukuru walipa kodi kwa maendeleo ya Zanzibar kwani kiwango cha fedha wanachochangia ndio kinachosaidia kuleta maendeleo ya nchi ikiwemo ujenzi wa barabara, maji, ujenzi wa skuli, hospitali na miundimbuni nyengine.
“Lengo letu la kuja hapa ni kuwashukuru na kuzungumza na nyinyi msituchoke sisi ni wenzenu na msitukimbie kwani lengo letu ni kuhakikisha mnafanyabiashara na mnapata faida kwani faida ndio itakayotuwezesha sisi kupata kodi”, alisema Kamishna huyo.
Aidha alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa jitihada anazozichukua za kuleta maendeleo makubwa kwa wananchi wa Zanzibar kupitia sekta za afya, elimu, miundombinu ya barabara na kuwaomba wananchi kuendelea kumuunga mkono kwa kulipa kodi kwa hiari.
Sambamba na hayo aliwataka wafanyabiashara kuwa mabalozi bora wa kulipa kodi ili kukuza maendeleo ya serikali na pia kuwapatia fursa vijana ambao wapo mitaani kuwafundisha namna ya kufanya biashara na kulipa kodi.
Naye Meneja Masoko wa Kampuni ya Aquart inayojishughulisha na uuzaji wa kahawa na vipodozi Zanzibar, Happiness Msangi, aliipongeza mamlaka hiyo kwa kuwatambua kuwa walipaji wazuri wa kodi jambo ambalo litawapa hamasa wafanyabiashara wengine waweze kulipa kwa wakati.
Alisema changamoto inayowakabili ni upande wa ulipaji wa kodi kutokana na biashara wanazofanya ni za kukopesha na muda wa kulipa kodi unapofika wanakuwa bado hawajakamilishiwa malipo na wateja wao.
Hivyo aliiomba ZRA iwaongezee muda wa kulipa kodi kutoka tarehe 5 hadi 30 ya mwisho wa mwezi ili waweze kulipa kwa usahihi na wakati na kuepusha usumbufu kwa mamlaka.
Kwa upande wake Meneja wa kampuni ya Al-hussein inayozalisha vifaa vya ujenzi, Joseph Matongo, alisema wanakabiliwa na changamoto ya ulipaji wa kielektroniki katika vifaa vya bandarini jambo linalowapotezea muda kwa kukaa sana sehemu ya malipo wanapotoka nje ya kisiwa kwa ajili ya kuchukua mizigo.