Skip to content

Dk. Samia awataka mawaziri kwenda na kasi ya mabadiliko

RAIS wa Jamuhuri ya Muungano wa TanzaniaDk. Samia Suluhu Hassan, ameitaka wizara ya mawasiliano na teknolojia kuhakikisha Tanzania nayo inakwenda sambamba na kasi ya mabadiliko ya dunia ya mawasiliano na teknologia na mkakati wa uchumi wa kidijitali wa kitaifa. 

Dk. Samia alieleza hayo jana baada ya kuwaapisha viongozi mbali mbali aliowateua Disemba 8, mwaka huu hafla iliyofanyika Ikulu ndogo Tunguu, Unguja.

Alisema dunia inakwenda na kasi ya mabadiliko hivyo wizara ya mawasiliano na teknolojia ya habari inapaswa kubadilika na kwenda na mabadiliko hayo ili kuona Tanzania haiachwi nyuma.

“Ukiutizama vizuri mkakati huu unataka shughuli ya peke yake. Uzoefu wangu toka tumeunda wizara hii tumeona nguvu kubwa inakwenda kwenye habari na huku kwengine mnafanya vizuri lakini hatuwendi kwa kasi ile ambayo tunatakiwa kwenda”, alisema.

Aliongeza kuwa; “Nimefanya hivi ili muelekeze nguvu kubwa kwenye teknologia ya habari na mawasiliano na mnajua mikakati yetu na miradi iliyopo elekezeni nguvu huko”.

Aidha Dk. Samia akizungumzia mawasiliano ya ndani na kimataifa, alisema kazi kubwa inatakiwa kufanyika ili kuifanya Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL) inasimama na kuwa shirika la kibiashara ya posta na simu Tanzania.

Alisema pia ipo kazi ya kuiunganisha Tanzania na nchi jirani kupitia mkonga wa taifa na kuwasisitiza kushughulika zaidi kwenye mambo hayo na kumtaka Waziri na timu yake kushughulikia jambo hilo.

Aidha aliwapongeza viongozi hao na kuwaambia amebandilisha nafasi zao kwa nia ya kuongezea ufanisi ndani ya serikali  na kuwataka kuwatumia Makatibu Wakuu na wataalamu watakaowakuta ili waweze kutekeleza majukumu yao vizuri.  

Akizungumza na Mabalozi, Dk. Samia aliwataka kwenda kuiwakilisha vyema Tanzania hasa katika upande wa kisiasa kwa kuzingatia kuwa baadhi yao watakwenda katika maeneo yenye kikiri na ndio maana wengi wao ni askari.

Vilevile Dk. Samia aliwakata mabalozi hao kwenda kuiwakilisha vyema nchi hasa kwa kuzingatia kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi sita zilizoongoza mapambano ya kudai uhuru Afrika lakini zipo nchi ambazo hali zao kisiasa sio nzuri ikiwemo Msumbiji na maeneo mengine hivyo aliwataka kwenda kuwekeza nguvu kuhakikisha Tanzania inasimama vyema.

Akimkaribisha Rais Samia, Makamu wa Rais, Dk. Philip Isdor Mpango, alisema viongozi waliokula kiapo na viongozi wengine wote wana kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba yale ambayo Watanzania wanataka basi wanayatekeleza kikamilifu kuendana na ilani ya CCM watakapoingia kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Alisema Rais Samia imempendeza kufanya mabadiliko katika timu yake ya ushindi hivyo aliwasihi kwenda kufanya kazi yao kwani kiongozi wao anawatarajia na watanzania wote.

Hivyo aliwasihi kushirikiana na viongozi wanaowakuta katika sehemu zao za kazi walioteuliwa na kwenda kucheza kama timu ya ushindi na kuheshimu mawazo ya wataalamu wanaowakuta katika nafasi hizo ili waweze kushinda na kuwaletea ushindi wananchi wa Tanzania.

Kwa upande wa Mabalozi aliwasisitiza kuifanyia kazi ajenda kuu ya diplomasia ya kiuchumi kuifanya vyema ili jitihada za Rais Samia kupitia falsafa ya R4 iweze kutekelezwa kikamilifu.

Aidha Dk. Mpango alimpongeza Rais Samia ambaye pia ni mwenyekiti wa wa chama cha mapinduzi (CCM) taifa, kwa ushindi wa chama hicho katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwani matokeo hayo yanatoa sura nzuri wanapokwenda.