RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema aliahidi kukabiliana na changamoto zinazoathiri maendeleo na haki za wananchi wakati serikali ya awamu ya nane anayoiongoza ilipoingia madarakani.
Alitaja miongoni mwa changamoto hizo kuwa ni rushwa, matumizi mabaya ya rasilimali za umma, uzembe, kukosekana kwa uwajibikaji katika utumishi wa umma, kutozingatiwa kwa sheria na ukiukwaji wa maadili ya utumishi ya umma.
Dk. Mwinyi alieleza hayo jana wakati wa maadhimisho ya miaka miwili ya Taasisi ya Rais Ufatiliaji na Usimamizi wa Utendaji Serikalini Zanzibar (ZPDB), yaliyofanyika katika viwanja vya Ikulu Mjini Zanzibar.
Alisema katika kufanikisha dhamira hiyo, alianzisha taasisi hiyo ili kufuatilia na kusimamia utendaji wa serikalini, lengo likiwa ni kuongeza tija na ufanisi kwenye utoaji wa huduma za afya, elimu, maji, umeme, uwezeshaji wananchi kiuchumi, utamaduni, michezo na usafirishaji.
Dk. Mwinyi aliongeza taasisi za ufuatiliaji kama PDB, sio ngeni duniani na zipo taasisi zinazofanana nazo zilizoundwa kwa dhamira ya kusaidia kufanikisha utendaji na malengo ya serikali katika kuleta maendeleo ya nchi.
Aliongeza kuwa ameridhika na usimamizi wa vipaumbele vyote kwa sekta usimamizi ambao unalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kuhakikisha maeneo ya vipaumbele yanapata mafanikio.
Alisema pamoja na mafanikio yaliyopatikana bado kazi kubwa inahitajika ili kuondokana na tabia iliyojengeka ndani ya vyombo vya serikali hasa kwa watumishi kufanya kazi kwa mazoea, kutokuwa na kuchukua muda mrefu kwa kazi inayoweza kufanyika kwa kipindi kifupi.
Awali akimkaribisha Dk. Mwinyi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu, Ali Suleiman Ameir ‘Mrembo’, alisema akiwa msimamizi wa taasisi hiyo anaridhika na utendaji kazi kwa uwajibikaji wake na busara za watendaji wake.
Alieleza kuwa mambo hayo yamesaidia kutumia muda mdogo kufanya ufuatiliaji na kusimama sambamba na kusifu maendeleo ambayo yamepatikana ndani ya miaka miwili ya taasisi hiyo.
Mapema Ofisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Prof. Mohammed Hafidh Khalfan, alisema wapo baadhi ya viongozi wanaokwamisha jitihada za taasisi hiyo kwa kutotoa mashirikiano ambayo yanapelekea kuzorota kwa ufatiliaji katika baadhi ya miradi.
“Baadhi ya viongozi hujaribu kuingilia utendaji wa taasisi jambo ambalo halipendezi, kwani baadhi ya viongozi hutuchukulia kama ni watafutaji wa makosa tu na hivyo kutotoa ushirikiano unaohitajika”, alieleza Prof. Khalfan.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Codfrey Nyamrunda na Mwakilishi wa Taasisi ya Tony Blair (TBI), Layla Ghaid, walimpongeza Dk. Mwinyi kwa ubunifu wake uliopelekea kuanzishwa kwa chombo hicho kilichosaidia kusukuma kasi ya kutekeleza miradi oliyoahidiwa kwa wananchi wa Zanzibar.
Hivyo waliahidi kuendelea kushirikiana pamoja kuhakikisha ZPDB inafikia malengo iliyojiwekea kwa ufanisi mkubwa na kuunga mkono katika juhudi zake za kuwatumikia wananchi wa Zanzibar.