Skip to content

Dk. Mwinyi: Nimeridhika viwango vya ubora Amaani Complex 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema ameridhika na viwango vya kisasa vilivyofikiwa katika ujenzi hoteli ya New Amani Complex na mikahawa iliyokuwepo katika uwanja huo kwani vimefikia viwango vya kimataifa.

Dk. Mwinyi alieleza hayo mara baada ya kufungua maduka, mikahawa, ukumbi wa mikutano na hoteli katika uwanja wa New Amani Complex ambapo ni awamu ya pili ya ukarabati wa uwanja huo.

Alisema hoteli hiyo ina viwango vizuri na vya kimataifa hivyo mtu anayetoka sehemu yoyote iwe ndani ama nje ya Zanzibar, anaweza kuitumia kutokana na ubora wake.

Aidha alisema mbali na hoteli hiyo, pia kuna ukumbi wa mikutano wa kisasa wenye sifa zote, hivyo watu wawe tayari kuutumia kwa mikutano mbalimbali. “Zanzibar hivi sasa nasi tunajivunia kuwa na kumbi za kimataifa”, alisema Dk. Mwinyi.

Dk. Mwinyi alisema uwanja huo utakuwa umekamilika kwa kila kitu ikiwemo hoteli, maduka ukumbi wa mikutano mikahawa, maegesho na viwanja vya mpira, hivyo ni lazima kutuumia kwa kufanya matamasha ili maeneo hayo yatumike vizuri.

Alitumia nafasi hiyo kuipongeza kampuni ya ORKUN Limited kutoka nchini Uturuki kwa kazi nzuri waliyoifanya katika ujenzi huo na viwango vya hali ya juu.

Akizungumzia kauli mbiu ya miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 inayosema, ‘Amani, Umoja na Mshikaamno kwa Maendekeo ya Taifa Letu’, Dk. Mwinyi alimshukuru Mwenyezimungu kwa kuendelea kuwapa wananchi wa Zanzibar amani, umoja na mshikamano.

Naye Waziri wa Habari, Vijana, Utakaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita, alimpongeza, Dk. Mwinyi kwa jitihada anazozichukua katika kuibadilisha New Amani Complex na kuendelea kuipatia heshima Zanzibar kwa mambo makubwa ya maendeleo anayoyafanya kwa wananchi.

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Fatma Hamad Rajab, alisema ukarabati wa hoteli, ujenzi wa mikahawa, maduka, maegesho ya gari na ukumbi wa mikutano yote hayo ameyafanya ndani ya uongozi wake na anastahiki kuthaminiwa, kuenziwa na anastahiki kuvishwa taji la heshima.

Alimpongeza kwa juhudi kubwa ambayo imewekezwa kupitia wizara hiyo ambayo ni jambo kubwa la kihistoria kwa Zanzibar.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi, Sabiha Filfil Thani, alimpongeza Dk. Mwinyi kwa kuiletea Zanzibar maendeleo ndani ya miaka minne ya mfano katika uongozi wake.

Alisema alipokuwa akiomba ridhaa, aliwaahidi wananchi yajayo ni neema na neema hiyo ya maendeleo wameiona katika kipindi kifupi cha uongozi wake na mwenye macho haambiwi tizama.

Naye Ilhan Karadeniz ni Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya ORKUN Limited kutoka Uturuki, alisema kazi iliyofanyika ni kubwa kwa majukumu ambayo alipewa ikiwemo ujenzi wa hoteli, mikahawa na ukumbi wa mikutano kwa muda wa miezi mitano na alifanya kazi hiyo usiku na mchana ili kuweza kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.

Aliipongeza serikali kwa kumuamini na kumpa nafasi ya kufanya kazi hiyo ambayo ameikamilisha kwa wakati uliotakiwa.