Skip to content

Chalamila akutana na viongozi wa wafanyabiashara Kariakoo

  • Bara

NA MWANDISHI WETU

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam,Albert Chalamila, amekutana na wadau wa biashara katika eneo la Kariakoo pamoja na taasisi mbalimbali ikiwemo TANESCO, TANROAD, LATRA, DAWASA, taasisi za fedha na kamati ya usalama ya mkoa

Pamoja na mambo mengine kikao hicho kilijadili masuala mbalimbali yenye lengo la kuimarisha biashara Kariakoo unaokidhi viwango hususani hali ya usalama ambayo itawezesha biashara kufanyika saa 24.

Aliipongeza halmashauri ya jiji kwa kuanza mchakato wa ununuzi wa kamera ambazo zinatarajiwa kufungwa maeneo mbalimbali ya mitaa ya Kariakoo.

Aidha katika kupunguza msongamano eneo hilo, Chalamila alisema kupitia kikao hicho wamejadili mpango shirikishi wa kuzuia gari,bajaji na pikipiki kuingia katikati ya mitaa ya Kariakoo wakati wa asubui, mchana na jioni. 

Alisema eneo la Kariakoo ni muhimu kibiashara kwani linahudumia Tanzania na nchi jirani,hivyo gari zitaruhusiwa kuingia usiku pekee ili kupunguza msongamano na kuruhusu biashara kufanyika bila usumbufu asubuhi hadi jioni

Sambamba na hilo, alisema wakati umefika kwa Kariakoo kuwa eneo maalum la biashara na mtu akitaka kufanya biashara lazima awe amekidhi vigezo vitakavyowekwa.      

Katika hatua nyingine, aliwataka wafanyabiashara na wadau wengine ikiwemo taasisi za fedha kuona namna ya kuongeza muda wa kufanya kazi hadi usiku hususani katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka ili kutoa fursa kwa wananchi kupata huduma kwa urahisi zaidi.

Aliliagiza jeshi la polisi kuimarisha ulinzi kwawafanyabiashara na wananchi katika kipindi hiki cha sikukuu kwa sababu kipindi kama hiki mahitaji ya bidhaa huongezeka kwa wananchi.