Skip to content

Dk. Mwinyi atunukiwa udaktari wa heshima wa uchumi

CHUO Kikuu cha Zanzibar (ZU), kimemtunuku shahada ya heshima ya uzamivu uchumi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa  Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi kutambua na kuthamini mchango  wa uongozi wake unaoacha alama  na historia wakati wote

Dk. Mwinyi alitunukiwa shahada hiyo jana wakati wa mahafali ya 22 yaliyofanyika katika viwanja vya chuo hicho Tunguu Zanzibar.

Akizungumza wakati wa mahafali hayo, Dk. Mwinyi alikishukuru chuo hicho kwa kuthamini juhudi na kazi zinazofanywa na seikali anayoiongoza kwa ajili ya maendeleo ya nchi na watu wake

Alieleleza kuwa shahada aliyotunukiwa itamuongezea kasi  ya utendaji na kumpa motisha ya  kuendelea kuwatumikia wananchi kwa kuwapelekea maendeleo katika nyanja mbali mbali.

“Shahada niliyotukiwa inaakisi kazi inayoifanywa na serikali ninayoiongoza na kwamba itaniongezea hamasa ya   kufanya kazi zaidi kwa maendeleo ya nchi na wananchi wetu”, alieleza Dk. Mwinyi.

Alifafanua kuwa amepokea shahada hiyo na kuwashukuru viongozi na watendaji wote serikalini kwa kumuunga mkono na kumpa ushirikiano unaofanikisha kufikiwa kwa malengo ya maendeleo ya nchi.

Hivyo aliahidi kuienzi heshima aliyopewa na chuo hicho  na kuwahakikishia wananchi kuwa ataendelea  kuwatumikia  wananchi  uwezo wake wote na kwamba shahada hiyo sio mwisho wa safari bali mwanzo wa hatua kubwa ya maendeleo katika miaka ijayo

Akisoma Wasifu wa Dk. Mwinyi, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, Dk. Maryam Jaffar Ismail, alimuelezea Dk. Mwinyi kuwa ni kiongozi wa mfano anayewajali watu wake  pamoja na maendeleo ya nchi.

Dk. Maryam aliainisha mafanikio yaliyopelekea Baraza hilo kuridhia kutunuku shahada hiyo ni pamoja na uimarishaji wa miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege  hatua inayochochea ongezeko la watalii na fursa za ajira katika sekta hiyo kwa wananchi

“Maeneo mengine ni kuimarika kwa sekta ya uchumi wa buluu  na matumizi sahihi ya rasilimali ziliopo nchini, uwezeshaji wa wanachi kiuchumi ikiwemo kuwapatia mikopo ili kuinua kipato chao na ongezeko la bajeti ya serikali  na pato la taifa pamoja na  kudhibiti kasi ya  mfumuko wa bei”, alieleza Makamu Mwenyekiti huyo.

Aliongeza kuwa maeneo mengine yaliyozingatiwa kuwa ni  kuanzishwa kwa miradi ya  kimkakati inayosaidia  kukuza kwa  uwezo wa wananchi  na maendeleo ya kiuchumi, ongezeko la pensheni jamii kwa  wazee na  uanzishwaji wa mfumo wa ufuatiliaji  wa ukaguzi wa ndani katika taasis za umma .

Dk. Maryam pia alieleza kuwa ujenzi wa skuli za ghorofa na  kuimarika kwa maslahi ya  walimu, skuli za ufundi na elimu jumuishi pamoja na kuimarika kwa sekta ya afya  kwa ujenzi wa hospitali za mikoa  na wilaya katika wilaya zote za Zanzibar na  ujenzi wa  viwanja vya michezo vya New Amani Complex na Gombani Pemba. 

Maeneo mengine yaliyotajwa ni uchimbaji wa visima vya maji na uanzishwaji wa mfumo wa ‘Sema na Rais’ uliochangia kwa kiasi kikubwa kutatua matatizo ya wanachi na kupatiwa ufumbuzi.

Katika mahafali hayo, jumla ya wahitimu 1,078 kati yao wanawake 690 na wanaume 458 walitunukiwa shahada ya kwanza, shahada ya uzamili na stashahada katika gfani mbali mbali ikiwemo ya sheria, biashara, sayansi na uhandisi.