Skip to content

Dk. Mwinyi : serikali kuwafidia nyumba wanaopisha miradi ya maendeleo

RAIS wa  Zanzibar na Mwenyekiti wa  Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuanzia sasa serikali  itawafidia nyumba bora wananchi wanaotoa maeneo yao kupisha miradi ya maendeleo.

Rais Dk. Mwinyi amefahamisha  kuwa Serikali imedhamiria  na jukumu la msingi la kuhakikisha wananchi wanapata makaazi bora ya kuishi.

Alieleza kuwa  kumekuwa na baadhi ya wananchi wanaoendelea kujenga nyumba zisizo na ubora (vibanda) licha ya kufidiwa fedha za kutosha na Serikali.

Rais Dk. Mwinyi alisema hayo juzi alipozindua mradi wa mauzo wa nyumba za Chumbuni zinazojengwa na Shirika la Nyumba Zanzibar  (ZHC) , ukumbi wa mikutano wa hoteil ya Amani, mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.

Rais Dk. Mwinyi amefahamisha kuwa jitihada hizo zimekuwa endelevu kwa awamu tofauti  zilizoanza  baada ya Mapinduzi ya Januari 1964  Chini ya Uongozi wa Hayati Abeid Aman Karume.

Aidha Dk. Mwinyi aliwahakikishia wananchi kuwa serikali itaendelea  kutafuta fedha zaidi za kuuendeleza Miradi mikubwa ya Ujenzi wa Nyumba za Maakazi maeneo mbalimbali.

Aidha Rais Dk. Mwinyi amezisitiza taasisi za kifedha ziliopo kufanya kazi kwa ukaribu na Shirika la  nyumba la Zanzibar ili kufanikisha azma hiyo.

Alifahamisha kuwa  ujenzi wa nyumba bora za makaazi  unaenda sambamba na  uimarishaji  wa miji bora  na  barabara zitakazotoa taswira  nzuri ya nchi na kutoa  rai kwa Wananchi kuhamasika kununua nyumba hizo ili kuwa na Makaazi bora na ya kisasa.

Hata hivyo, Dk. Mwinyi amelisisitiza Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC) kuendelea kutafuta soko la nyumba zinazojengwa kwani ni wajibu  pamoja na kuwa na nyumba nyengine za kuwakodisha wananchi.

Rais Dk. Mwinyi alifahamisha kuwa ni vyema kwa wananchi kununua nyumba hizo hivi sasa kwa  maeneo yanayojengwa  yatakuwa na biashara nyingi baadae Pamoja na shughuli za kijamii na  barabara za uhakika.

Ameishauri taasisi kutoka  Sekta Binafsi kushirikiana na Shirika la Nyumba ili lipate mafanikio zaidi.

Rais Dk. Mwinyi pia aliipongeza taasisi ya ‘Infinity Group of Companies’ kwa wazo la kuwekeza Zanzibar  na  mpango wao wa kuwajengea uwezo Vijana wa Zanzibar kwenda kujifunza nchini Dubai  ili kuleta uzoefu huo Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi ameeleza kufarijika na kasi ya utendaji wa Shirika la Nyumba hivi sasa kwani limekuwa likitekeleza Miradi yenye tija badala ya kushughulikia Migogoro ya Nyumba kwa Muda mrefu.

Pia alitumia fursa hiyo kuwahimiza Watendaji wa sekta ya umma wanaokabidhiwa majukumu kuhakikisha wanaacha alama   katika maeneo yao ya kazi yatakayowajengea heshima wakati wote.

Akitoa taarifa ya kitaalamu ya mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzbar, Sultan Said alileza kuwa Mradi huo ni Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020-2025 ya kuimarisha nyumba za Makaazi .

Aliongeza kuwa mradi wa Chumbuni utakuwa na nyumba 3,000 na shirika linakusudia kuendeleza Miradi mikubwa ya kimkakati ya Ujenzi wa Nyuma maeneo ya Kikwajuni, Kwa Mchina Unguja, Kisakasaka na Mabaoni Mfikiwa Pemba.

Naye Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi, Rahma Kassim Ali, alieleza kuwa kuanzishwa Idara ya Maendeleo ya Makaazi  kutaleta chachu ya utekelezaji wa  Sera ya Makaazi itakayoleta Mafanikio makubwa  hapo baadae.

Alibainisha kuwa Wizara bado ina maeneo mengi  yaliotengwa kwa ajili ya Maendeleo ya Makaazi  ili kufanikisha dhamira ya Serikali ya kuwa na Miji Bora.