RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar imepiga hatua kubwa kwenye kukidhi ukuaji wa sekta ya usafiri wa anga.
Dk. Mwinyi ameeleza hayo jana katika ukumbi wa hoteli ya Verde alipokuwa akifungua kongamano la sita la usafiri wa anga kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alisema kwenye sekta ya usafiri wa anga serikali imefanikisha miradi kadhaa, ambapo lengo kubwa ni kuongeza ufanisi kwa wasafiri sambamba na kukuza utalii ambao ni sekta yenye umuhimu mkubwa kiuchumi.
Dk. Mwinyi aliwaeleza washiriki wa kongamano hilo kwamba sekta ya usafiri wa anga ina nafasi kubwa katika kukua kwa utalii, hivyo serikali itaendelea kuwekeza kweye sekta hiyo kutokana na umuhimu wake.
Alisema miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana kwenye sekta ya usafiri wa anga hapa Zanzibat ni pamoja na kukamilika kwa ujenzi wa jengo la abiria ya ‘terminal iii’, ambalo kwa sasa linafanyakazi kwa ufanisi katika utoaji wa huduma.
Aidha alisema serikali imeanza ujenzi wa jengo jipya la abiria la ‘terminal ii’ lenye ukubwa wa mita za mraba 16,000, ambalo litakuwa na uwezo wa kuhudumia zaidi ya abiria 1,300,000 kwa mwaka.
Dk. Mwinyi pia alisema, serikali inatekeleza mradi wa ujenzi, ukarabati na uboreshaji wa jengo la ‘terminal i’ lililojengwa miaka ya 1950 pamoja na kutekeleza mradi wa ujenzi wa kituo cha biashara, kitakachojumuisha maduka, mikahawa, huduma za kibenki na ofisi.
Alieleza, serikali pia inatekeleza mradi wa ujenzi na utanuzi wa Uwanja wa ndege wa Pemba unaojumuisha utanuzi wa urefu wa njia ya kurukia ndege kutoka mita 1,525 hadi mita 2,510 na ujenzi wa maegesho ya ndege (apron) yenye uwezo wa kuchukua ndege mbili kubwa na ndege nane ndogo.
Dk. Mwinyi alieleza, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inazingatia mikataba yote ya usafiri wa anga ya kimataifa ili kuhakikisha ukuaji wa sekta hiyo unaendelea kuwa salama.
Alisema, serikali imeimarisha mradi wa masafa ya mbali (VHF) unaojumuisha ufungaji wa vituo 18 vipya na redio kwenye viwanja vya ndege 12 na uwekaji wa mifumo ya kinasa sauti katika viwanja vinne vya ndege, uwekaji wa mfumo wa kutua kwa ndege (ILS) kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.
Naye, waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi, Dk. Khalid Muhamed Salum alisema sekta ya usafirishaji wa anga inakisia zaidi ya abiria milioni tatu husafiri kwa anga kila siku kutokana na umuhimu wa haraka wa safari zake.
Hivyo aliwasihi washiriki wa kongamano hilo wakiwemo nchi wanachama kujadili kwa kina masuala ya usalama, gharama na ufanisi ili kuwe kupatikane tija kwa changamoto zilizomo kwenye sekta hiyo.
Kongamano la sita la usafiri wa Anga la Jumuiya ya Afrika Mashariki, umewakutanisha wadau kutoka nchi za Afika Kusini, Burundi, Jamuhuri ya Demokrasia ya Congo, Kenya, Ethiopia, Somalia, Sudai Kusini, Rwanda na mwenyeji Tanzania.