RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amerudia kutoa pole kwa waathirika wa mkasa wa kuporomoka kwa jengo la ghorofa katika eneo la biashara moitaa ya Kariakoo jijini Dar es salam.
Dk. Samia alieleza hayo jana alipotembelea eneo la ajali hiyo mara baada ya kuwasili nchini akitokea nchini brazil alipohudhuria mkutano wa mataifa tajiri G20 na kueleza kuwa tukio hilo linatoa ujumbe wa kuangalia usalama wa majengo yaliyopo katika eneo hilo.
Alisema taarifa ya tume ya uchunguzi na uhakiki wa majengo ya eneo hilo iliyoundwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, itawekwa bayana mara itakapomaliza kazi yake na kwamba itashauri hatua za kuchukuliwa hata kama za kubomoliwa kwa majengo yasiyo na sifa.
“Naambiwa kwamba mwaka 2013 kuna tume mbili zilifanya utafiti katika eneo hili na kutoa taarifa yao, sasa taarifa zile zitakwenda kutusaidia kwenye taarifa ambayo tunataka kuifanya”, alisema.
Alisema wakati anaonyeshwa jengo hilo inaonekana kuwa hapakuwa na usimamizi mzuri ambapo watu wametumia fedha chache kujenga jengo kubwa bila ya kufikiria madhara yanayoweza kutokea jambo linalopaswa kuepukwa.
“Kubomoka kwa jengo hilo kumetupa funzo kubwa, kama serikali sasa tunawajibika kuingia Kariakoo kuangalia umadhubuti wa majengo yetu”, aliongeza Dk. Samia.
Aliongeza kwa kumpongeza waziri mkuu kwa kutekeleza maelekezo aliyompa ya kuunda tume itakayofanya kazi hiyo na kwamba inasubiri maelekezo ili kuingia katika eneo hilo kwa ajili ya kuangalia ubora wa majengo.
Akizungumzia zoezi la uokozi, Dk. Samia alisema wakati vikosi vya uokozi na wadau wengie wakiendelea kusafisha ineo la ajali pamoja na kusimamisha zoezi hilo, waendelee kufukua kwa tahadhari kuona kama kuna watu walionaswa ili watolewe wakiwa hai wamefariki ili wakasitiriwe kwa heshima.
Vile vile Rais Samia alipongeza jitihada zilizochukuliwa na vikosi vya ulinzi na usalama, watoa huduma mbali mbai, wananchi pamoja na viongozi wa serikali zilizolenga kuokoa maisha ya watu walionaswa katika jengo pamoja na mali za wafanyabiashara na wamiliki wa naduka.
“Pamoja na jitihada zilizofanywa taarifa niliyopewa hadi saa tatu asubuhi ya leo (jana) tumepoteza wenzetu 20 na kuna majeruhi waliopelekwa hospitali na kutibiwa kisha wakaruhusiwa lakini wapo wanaoendelea na matibabu”, alisema Rais Samia.
Aidha aliwataka viongozi wa serikali kuu, serikali za mitaa na taasisi zinazosimamia ujenzi kuchukua hatua kuhakikisha matukio kama hayo hajirudii pamoja na kuzingatiwa kwa sheria.
Aidha aliwashukuru watanzania na wafanyakazi walioshirki zoezi hilo kwa kujielekeza kwa moyo kuwaokoa watu waliokuwemo ndani ya jengo hilo badala ya kujielekeza kuchukua mali kujunufaisha.
“Wakati tukiendelea na zoezi la kufukua na kuona kilichomo, mali zote tutakwenda kuzihifadhi na baadae tutawaita wenye mali kutembua mali zao”, alisema.
Wakati huo huo Rais Samia alikwenda katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuwajulia hali majeruhi waliolazwa hospitalini hapo na kuwaombea wapone kwa haraka.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Waziri Mkuu Kassim alisema kazi inaendelea katika jengo hilo pamoja na kuondoa zege kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo, wachimba madini na sekta binafsi ambao walitoa vifaa vya uchimbaji na magari ya huduma za dharura (ambulance) zilizosaidia katika kazi ya uokoji.