NA SAIDA ISSA, DODOMA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, jana alipiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa huku akihimiza amani na usalama.
Dk, Samia alipiga kura katika kitongoji cha Sokoine kijiji cha Chamwino ambapo alisema upigaji kura ni mtindo wa demokrasia katika kuwapata viongozi.
“Kura hizi ni mtindo wa demokrasia na ni utamaduni wetu wa kisiasa, tuufanye kwa salama na amani, tusivunje amani yetu, pigeni kura kwa maelewano na masanduku yanavyosema ndio hivyo matokeo yatoke,” alisema.
Alisema ni matumaini yake kwamba uchaguzi huo utahitimishwa kwa salama na kutoa nafasi kwa watanzania kuchagua uongozi wao katika ngazi za maeneo wanayoishi.
Mbunge wa jimbo la Chamwino na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi, aliwahimiza wakazi wa Chamwino kupiga kura kwa wingi.
Uchaguzi wa serikali za mitaa unafanyika kila baada ya miaka mitano na kwa mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2019.