Skip to content

Dk. Samia azindua mkakati matumizi nishati safi

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema umefika wakati kwa watanzania kutumia nishati safi ili kuiokoa nchini katika janga la uharibifu wa mazingira.

Dk. Samia alitoa agizo hilo jana wakati akizindua mkakati wa taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ya mwaka 2024-2034, hafla iliyofanyika katika kituo cha kimataifa cha mikutano cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Kutokana na  hali hiyo, Dk. Samia aliiagiza wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano kuandaa katazo la taasisi zote zinazohudumia watu zaidi 100 kutumia kuni na mkaa ifikapo mwezi Agosti mwaka huu.

Katika hafla hiyo, Dk. Samia alitoa maelekezo kadhaa ya utekelezaji wa mkakati huo, ikiwa ni pamoja na ndani ya miezi mitatu ijayo, waziri Mkuu Kassim Majaliwa awasilishe taarifa ya utekelezaji.

Agizo jengine ni kwa wizara ya Nishati ihakikishe inawafikishia mkakati wadau wote kwa kuweka katika tovuti na katika mitandao ya kijamii.

Aidha katika agizo jengine Dk. Samia aliagiza wizara ya Nishati ikae na wadau ikiwa ni pamoja na sekta ya umma na binafsi kubaini maeneo ambayo yakifanyiwa kazi yataongeza kwa haraka upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa gharama nafuu.

Pia aliitaka wizara ishirikiane na wadau kwa kuhakikisha wanakuwa na mfuko wa kuendeleza nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2025, na kwa kuanzia ndio kazi wanayokwenda kuifanya Paris nchini Ufaransa.

Alisema  wananchi  juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia hata hivyo kinachohitajika uhakika wa upatikanaji wa nishati hiyo, hivyo taasisi zinazohusika lazima zihakikishe huduma inakuwa endelevu.

Aidha alisema mkakati huo wa kitaifa utachangia jitihada za serikali kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kutokana na uharibifu wa misitu ambao huchangiwa na shughuli za kibinadamu.

Alieleza mbali na athari za kimazingira, lakini inakadiriwa kuwa watanzania zaidi 33,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na magonjwa ya kupumua, ambapo kwa kiasi kikubwa huchangiwa na uvutaji wa moshi wa kuni na waathirika wakubwa ni wanawake.

Alisema safari ya kimaendeleo haiwezi kupiga hatua kubwa kama asilimia 90 ya wananchi bado wanatumia nishati isiyorafiki kwa afya, mazingira na uchumi wananchi.

Kwa upande wake, waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoathirika na changamoto zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi na shughuli zinazochangia athari hizo ni matumizi nishati isiyokuwa safi ya kupikia.

Nae Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko alimpongeza Dk. Samia kwa kuwa kinara wa nishati safi ya kupikia barani Afrika hususani progamu ya nishati ya Safi ya kupikia kuwasaidia wanawake barani Afrika, ambayo inalenga kuwawezesha wanawake.