Skip to content

Mama Mariam: Maradhi ya saratani yanarejesha nyuma uchumi

MKE wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi amesema maradhi ya saratani ni hatari na yanarejesha nyuma juhudi za jamii na uchumi hata kusababisha umasikini kwa jamii kutokana na gharama kubwa za matibabu yake kwa wagonjwa wengi kutokuwa na uwezo wa kumudu matibabu.

Mama Mariam kwa huzuni aliyasema hayo Ofisini kwake Ikulu ya Migombani, mkoa wa Mjini Magharibi alipozungumza na wageni kutoka Hong Kong, Dk. Jeremy Hon, Daktari na Mtaalamu wa maradhi ya saratani aliyeambatana na Angel Hon wa taasisi ya ‘Belt and Road Creation Resources’ waliomtembelea ofisini kwake.

Mama Mariam Mwinyi ambae pia ni Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), aliwaeleza wageni wanavyofanyakazi na kuwa karibu na jamii kuwashajihisha watu kuimarisha afya zao ili kujiepusha na maradhi yasiyoambukiza yakiwemo kisukari, presha na moyo.

Aliueleza ugeni huo kwamba ZMBF katika kuisaidia jamii juu ya maradhi hatari yakiwemo ya saratani imekuwa na utaratibu wa kila baada ya miezi mitatu kuweka kambi za matibabu bure Unguja na Pemba kwa mikoa yote kuisadia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na wakuu wa mikoa kuwaalika wananchi kwaajili ya matibabu na uchunguzi wa afya zao.

Alisema kambi hizo zimesaidia kugundulika kwa kesi nyingi zikiwemo saratani za matiti zinazowasumbua kina mama wengi pamoja na maradhi mengine.

Aidha Mama Mariam alimualika Dk. Jeremy kuangalia uwezekano wa kuja Zanzibar kushirikiana na serikali kupitia Wizara ya Afya kwani serikali tayari imekamilisha hospitali 10 za Wilaya Unguja na Pemba na moja ya Mkoa pamoja na kuweka miundombinu imara na vifaa vya kisasa vya maabara.

Pia alieleza kuwa ZMBF imeendelea kuishajihisha jamii kufanya mazoezi kwa kuungana nao mara kadha kwenye matembezi ya hiari ili kuimarisha afya zao sambamba na kuisajihisha jamii juu ya umuhimu wa lishe bora kwa mama wajawazito na watoto.

Akiuzungumzia mradi wa ‘Tumaini Kit’ unaozalisha taulo za kike kwa ajili ya wasichana kupitia kiwanda chake kilichopo Mnara wa mbao, Mama Mariam alieleza wageni wake hao lengo la mradi huo ni kutatua changamoto za hedhi kwa wanafunzi wa kike zinazorudisha nyuma maendeleo yao ya elimu kwa Unguja na Pemba.

Alieleza kupitia mradi huo umewasaidia wasichana wengi hasa wa vijijini kuhudhuria skuli na kufanya vizuri kwenye masomo yao ambao awali wengi waliacha kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutomudu gharama za kujikimu kila wanapopata ada za mwezi.

Halikadhalika, Mama Mariam Mwinyi amebainisha kuwa mradi huo umelenga kuzalisha taulo za kike zaidi ya 20,000 kwa mwaka na hadi sasa tayari ZMBF imefanikiwa kusambaza kwa wanafunzi na wasichana zaidi ya 7000 wa skuli za msingi na sekondari kwa Unguja na Pemba.

Kwa upande wao Dk. Jeremy na Angel Hon walipongeza juhudi za maendeleo na kazi inayofanywa na ‘Zanzibar Maisha Bora Foundation’ na kueleza shauku yao ya kutaka kuendeleza ushirikiano wao na Zanzibar hasa katika kubadilishana uzoefu kwenye sekta ya afya kupunguza wimbi za maradhi ya saratani yanayowasumbua wananchi wengi.