NA MWAJUMA JUMA
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Riziki Pembe Juma amesema ujenzi wa viwanja vya michezo ni ishara ya mafanikio katika maendeleo ya michezo Zanzibar.
Aliyasema hayo wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi katika mradi wa michezo ya ndani ujulikanao michezo kwa maendeleo ‘sports for development’, huko skuli ya Regeza Mwendo, ikiwa ni miongoni mwa maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na wadau wa michezo, katika kuimarisha sekta ya michezo na kuendelea kuwawezesha vijana wao kuweza kushiriki katika michezo mbali mbali.
Hata hivyo alisema ujenzi wa viwanja hivyo pia utanufaisha skuli mbali mbali za maeneo ya karibu na jamii.
Alisema utekelezaji wa mradi huo unakwenda sambamba na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 – 2025, kwa kuihamasisha jamii kushiriki katika michezo yote ya kisasa na ya asili.
Mapema Kamishna wa Idara ya Michezo Zanzibar Ameir Mohammed Makame alisema mradi huo unajumuisha ujenzi na ukarabati wa viwanja sita vya mpira katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba na kila kiwanja kitakuwa na uwezo wa kuchezwa michezo minne kwa nyakati tofauti.
Alisema mradi huo una lengo la kujenga na kukarabati viwanja vya michezo vinavyozingatia usawa wa kijinsia na kuzingatia watu wenye ulemavu.
Aidha alisema kwa sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 50 kwa maeneo yote ya Unguja na Pemba na katika mwaka huu wa fedha 2024/2025 mradi umetengewa jumla ya shilingi 633,982,000 kutoka kwa washirika wa maendeleo ‘Shirika la maendeleo la Kimataifa la Ujerumani ‘( GIZ).
Maeneo yaliyobahatika kupitiwa na mradi huo ni pamoja na Tumbatu, Chuo cha Ufundi wa Amali Mkokotoni na Mwera Rejeza Mwendo kwa Unguja na kwa Pemba ni Mchangamdogo, Kangani na kiwanja cha Tennis Chake Chake.