ASYA HASSAN NA MWAJUMA JUMA
BADHI ya wananchi waliohudhuria na kupata mgao wa samaki Jodari katika tamasha la vumba lililofanyika sambamba na shughuli mbali mbali wameeleza kufurahishwa kwao na ubunifu ulioonesha na waandaaji wa tamasha hilo.
Wakizungumza katika viwanja na fukwe za Kizingo mjini Unguja, wananchi hao walisema hatua hiyo muhimu kwani imesaidia kuonesha jinsi rasilimali za bahari zinazopatikana kwenye bahari ya zanzibar zinatumika kwa manufaa ya wote na kuonesha kujali wananchi.
Miongoni mwa wananchi hao, Zaituni Abdullah (46) kutoka Kwarara, alisema serikali ya awamu ya nane imechukua hatua stahiki ya kuwasaidia wananchi kupata samaki jamboambalo hukonyuma halikuwahi kutokea.
Alisema hapo awali hawakuamini kama watapewa kweli samaki lakini kupitia hatua hiyo imewapa moyo ya kuonesha kwamba kweli serikali ya awamu ya nane inawajali wananchi wake.
“Ni jambo la kushukuru kuona serikali ya awamu ya nane inafanya juhudi za kuboresha maisha ya wananchi hatua inayoleta matumaini makubwa kwa wananchi wa visiwa hivi katika kupata maendeleo makubwa zaidi katika siku zijazo”, alisema Zaituni.
Alisema sherehe za mapinduzi zimekuwa zikifanyika kila mwaka lakini hawajawahi kuona neema hizo hivyo kupitia zoezi hilo wanathamini juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa kufanya mabadiliko yanayoleta neema kwa wananchi.
Hata hivyo alifahamisha kuwa ni jambo zuri kuona viongozi wakifanya maamuzi yanayowaletea wananchi maendeleo na furaha kwani itasaidia kuboresha maisha ya wananchi.
“Kusema kweli tumekuja kama kubahatisha tu, maana nilidhani yanayotangazwa sio ya kweli, lakini kumbe imekuwa kweli nasi tumekuwa wanufaika”, alisema Zaituni.
Naye Hakim Hassan kutoka Fuoni alisema ugawaji wa samaki na majiko ya gesi ya kupikia ni uthitirisho wa kauli ya Dk. Mwinyi aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi ya ‘Yajayo ni neema tupu’.
“Ni mategemeo yangu kwamba kupitia uongozi wa Rais Mwinyi katika miaka mitano ijayo kutakuwa na mafanikio zaidi kupitia nyanja mbali mbali za kiuchumi na kijamii”, alieleza Hakim.
Kwa upande wake, Jamila Mohammed kutoka Nyarugusu, alisema serikali imefanya vizuri kutoa samaki kwa wananchi lakini kuna baadhi ya watu wamejitokeza kuwatepeli wananchi kwa kuwataka kulipa kulipa fedha na kuwaandika namba mkononi ili kuwapatia samaki jambo ambalo sio sahihi.
“Nadhani mwakani kuna haja ya waandaaji kuweka kuweka utaramibu mzuri zaidi kama wataamua kugawa tena samaki katika tamasha hili ili kuwadhibiti watu wasio na nia njema maana hao hawakosekani”, alishauri Jamila.
Akizungumzia zoezi hilo mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Shaaban Ali Othman, alieleza kuwa katika tamasha wananchi wamegaiwa samaki Jodari na majiko ya gesi.
Alieleza kuwa tamasha hilo liliandaliwa kwa pamoja na wizara yake, Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) na Kamisheni ya Utalii Zanzibar limekusanya shughuli mbali mbali ikiwemo mashindano ya resi za ngalawa, kugawa samaki na burudani ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za miaka 61 ya mapinduzi.