LUANDA, ANGOLA
MAZUNGUMZO yaliyopangwa kufanyika ya kuwakutanisha rais wa Rwanda na Jamhuriya Kidemokrasia ya Congo DRC nchini Angola, kwa ajili ya kumaliza mgogoro wa mashariki mwa DRC, yamefutwa.
Maofisa wamesema kuwa, kulikuwa na matarajio makubwa kwamba, marais wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wangelikutana juzi kwa mualiko wa Rais wa Angola.
Hata hivyo, mazungumzo hayo yamefutwa. Mkuu wa ofisi ya Rais wa Angola aliwaambiawaandishi wa habari kwamba kinyume na matarajio, mkutano umeshindwa kufanyika.
Kwa upande wake ofisi ya rais wa DRC imesema kuwa, mazungumzo hayo hayakufanyikakutokana na masharti yaliyowekwa na Rwanda.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa Rwanda imeitaka DRC ifanye mazungumzo na waasi wa M23 sualaambalo nchi hiyo haijapanga kufanya na imeishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi hao.
Awali, Rwanda ilikuwa imethibitisha kwamba Rais Paul Kagame atashiriki katika mkutano huo akiambatana na waziri wake wa mambo ya nje, Olivier Nduhungirehe.
Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pia ilithibitisha kwamba Rais FelixTshisekedi atashiriki katika mazungumzo hayo, licha ya awali kukataa kufanya mazungumzo na Rwanda na kutoa mwito wa kuwekwa vikwazo vya kimataifa dhidi ya jirani yake huyo.
“Nchi yetu inaendelea kukabiliwa na uasi, ikiwa ni pamoja na uvamizi wa jeshi la Rwanda na magaidi wa M23,” alisema Tshisekedi wakati akihutubua bunge la nchi yake Jumatano iliyopita, akiwaita wanamgambo hao na nchi ya Rwanda kuwa “maadui wa Congo DR.”
Rais wa Angola, Joao Lourenco, aliyeteuliwa na Umoja wa Afrika kuwa mpatanishi, ameelezamatumaini kwamba Rwanda na DRC zinaweza kufikia makubaliano ya amani.