Skip to content

Shilingi 40.5 bn/- kuimarisha maeneo ya miji  

ZAIDI ya shilingi bilioni 40.5 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa mradi wa uimarishaji wa maeneo ya mji wa Unguja.

Katibu Mkuu wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Dk. Juma Malik Akili, alisema hayo alipokuwa akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa kuyapa hadhi maeneo ya mji yanayokua kwa haraka.

Zoezi hilo lilifanyika katika ukumbi wa Tume ya Mipango ambapo kwa upande wa wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, saini ilitiwa na Katibu Mkuu huku kampuni ya ujenzi wa mradi huo CRJE saini ilitiwa na meneja wa kampuni hiyo, Xu Cheng.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Akili alisema hatua hiyo pamoja na mambo mengine itaweza kuimarisha hali ya maisha ya wananchi kwa kuchochea utoaji wa huduma bora kwa jamii ili kukuza maendeleo ya kiuchumi.

Alisema mradi huo unatekelezwa kupitia mradi wa ukuzaji uchumi Jumuishi Zanzibar (BIG-Z) ambao unalenga kuimarisha hali ya maisha ya wananchi kwa kuweka usalama na kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Alisema utekelezaji wa mradi BIG – Z, utahusisha maeneo matatu ikiwemo maendeleo ya mijini na miundombinu jumuishi kama vile ujenzi wa barabara, masoko, sehemu za kitaliii na huduma nyengine, hivyo kupitia hatua hiyo ni moja ya utekelezaji wake.

Katibu huyo alisema hatua hiyo itakuwa chachu ya kurahisisha usafiri wa barabara na kuondosha maji yanayotuama katika makaazi ya wananchi ambayo yalikuwa yakisababisha athari mbalimbali ikiwemo wananchi kuyahama makaazi yao kipindi cha mvua.

Alisema ujenzi huo utahusisha kuyapa hadhi na kuyakuza maeneo ya mjini kwa kujenga na kukarabati mitaro ya maji ya mvua yenye urefu wa kila mita 4.76 katika manemba mbalimbali ya Mkoa wa Mjini Magharibi. 

Aidha alifahamisha kuwa mradi huo utaimarisha maeneo ya wazi kwa kufanya uboreshaji wa viwanja vya mpira pamoja na ujenzi wa barabara za ndani zenye urefu wa kila mita 9.14 kwa kuwekewa taa zinazotumia nguvu ya jua.

Hata hivyo alisema mradi huo pia utahusisha ujenzi wa masoko ya wajasiliamali ili kuwawezesha wananchi kufanya biashara zao kwa kujinafasi ili kukuza kipato chao.

Mbali na hayo alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi watakaopitiwa na mradi huo kuhakikisha wanatoa ushirikiano wa hali na mali pale ujenzi huo utakapoanza ili kufanikisha zoezi hilo kufanyika vyema na kumalizika kwa wakati.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Ukuzaji Uchumi Jumuishi Zanzibar (BIG-Z), Ali Juma Hamad, alisema ujenzi huo unatarajiwa kuchukua muda wa miezi 18 ambapo hivi sasa wanajiandaa kulipa fidia.

Meneja wa Kampuni ya CRJE, Xu Cheng aliishukuru serikali kwa kuwaamini na kuwapa mradi huo na kuahidi kwamba kazi hiyo wataifanya kwa uweledi na ufanisi ili kuweka mazingira mazuri ya maeneo hayo ili wananchi kuishi kwa amani.

Mradi wa uimarishaji wa miji Unguja unatekelezwa katika shehia 16 ziliopo ndani ya Mkoa huo zikiwemo Meya, Magomeni, Sebleni, Kwawazee, Nyerere na Muungano.

Maeneo mengine ni Sogea, Jang’ombe, Mpendae, Madema, Amani, Kilimahewa juu, Kilimahewa bondeni, Mapinduzi, Mkele, Shaurimoyo, mradi ambapo unatarajia kuwafikia wananchi 346 wa maeneo hayo.