Skip to content

Mkataba kuimarisha miundombinu, huduma za maji wasainiwa

NA AMEIR KHALID

WIZARA ya Maji, Nishati na Madini imetilia saini mkataba kwa ajili ya uendeshaji, usimamizi na uboreshaji wa miundombinu na huduma za maji safi na salama Zanzibar baina ya SMZ na kampuni ya Rand Water ya Afrika Kusini.

Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo ilifanyika jana katika ukumbi wamikutano wa jengo la Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (ZURA) Maisara ambapo viongozi mbali mbali wa ZAWA na wizara hiyo walishuhudia.

Akizungumza Waziri wa wizara hiyo, Shaib Hassan Kaduara, alisema wizara inaendelea kutekeleza miongozo na maelekezo yanayotolewa mara kwa mara kutoka serikalini ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora na endelevu za maji safi na salama.

Alisema serikali imesaini mkataba huo chini ya usimamizi wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji na Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar itakayokuwa msimamizi wa mkataba huo kwa upande mmoja na kampuni ya Rand Water kwa upande wa pili.

Aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliiagiza Wizara hiyo kuanza mchakato kutafuta kampuni yenye vigezo stahiki vya usimamizi na uendeshaji wa ZAWA na wizara ilianza mchakato wa kuandaa nyaraka, kutangaza na kupokea maombi ya wazabuni.

Alizitaja kazi nyengine kuwa ni kuchambua pamoja na kumpata mzabuni mmoja kati ya wazabuni waliomba ambaye ni Rand Water ya Afrika ya Kusini.

Aliongeza kuwa pamoja na majukumu mengine, kampuni ya Rand Water itakuwa na majukumu ya msingi kuimarisha  upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa maeneo yote Unguja na Pemba, kuimarisha miundombinu ya maji kwa kufanya marekebisho, ukarabati na upanuzi wa mifumo ya ugavi wa miradi ya maji iliyopo.

Majukumu mengine ni kujenga mitambo mipya ya kutibu maji na mitandao ya usambazaji maji, kuimarisha ufanisi wa uendeshaji kupitia mifumo ya kisasa ya usimamizi wa maji, kuwajengea uwezo wafanyakazi wa ndani kuhusu mbinu bora na za kisasa za uendeshaji wa mifumo ya maji na kuwekeza miradi mipya ya maji Unguja na Pemba bila ya kuathiri utekelezaji wa miradi mengine ya wafadhili.

Alifafanua kuwa utekelezaji wa kazi za kampuni hii hautakinzana na utekelezaji wa miradi mengine ya maendeleo itakayofadhiliwa na washirika wa maendeleo badala yake miradi hiyo itasaidia malengo ya Serikali sambamba na kufikiwa kwa lengo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wote wa Zanzibar.

Alisema imetiliana saini na kampuni hiyo kwa kujiridhisha baada ya  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilipatiwa msaada wa kuthibitisha taarifa zinazohusiana na kampuni hiyo kupitia ubalozi wa Tanzania nchini Afrika ya Kusini.

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nishati na Madini Joseph Kilangi alisema kushirikisha sekta binafsi kwenye maji ni kuleta ufanisi zaidi katika sekta ya maji.

Alisema sera ya serikali kushirikisha sekta binafsi  katika  mambo mbali mbali ili kuona miradi mingi inafikiwa maelngo.

Kwa upande Afisa Mtendaji  Mkuu wa kampauni hiyo, Vusi Kugheka, alisema watahakikisha wanafaya vyema katika kutekeleza makubalianoa hayo ili lengo la serikali liweze kufikiwa.

Alisema kampuni yake ina uzoefu mkubwa katika sekta hiyo hivyo amaewataka wazanzibari kuondosha wasi wasi na watahakikisha wananchi wote wanapata maji.