Skip to content

CCWT yapongeza ongezeko bajeti ya mifugo, uvuvi

  • Bara

NA SAIDA ISSA, DODOMA

CHAMA cha wafugaji Tanzania(CCWT) kimeipongeza serikali na bunge kwa kuongeza bajeti ya wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2024/25 kiasi shilingi bilioni 460.3 kutoka bilioni 169 kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Mwenyekiti wa CCWT, Mrida Mshota alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo alisema kuwa hotuba hiyo imesheheni mambo mengi mazuri ikiwemo unenepeshaji wa mbuzi.

Mshota alisema wafugaji tunaipongeza serikali pamoja na bunge kuipitisha na kutuongezea bajeti yetu kwa kiasi kikubwa, kwani katika kipindi cha miaka mitatu ya Dk. Samia ameipa msukumo sekta hiyo.

“Katika bajeti hiyo wafugaji wengi wamehudhuria na kufurahia namna bajeti ilivyosheheni mambo mengi mazuri yatakayokuwa ni neema kwetu”, alisema mwenyekiti huyo.

Aidha mwenyekiti huyo alisema kuwa serikali imefungua mradi mkubwa wa unenepeshaji wa mbuzi tariri kongwa ambapo majengo hayo yaliyojengwa yanagharimu kiasi cha shilingi bilioni 1 na milioni 600.

Kwa upande wake chifu wa wamasai anayeongoza mikoa sita Matayani Simanga aliishukuru serikali inayoongozwa na Dk. Samia kwa kuendelea kuwatambua wafugaji waliopo nchini kwani Serikali inawaunga mkono.

Alisema kuwa ipo haja ya viongozi kutembelea maeneo ya wafugaji ili kubaini na kuzitatua changamoto walizonazo kwani wafugaji bado wapo nyuma katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Wafugaji wengi bado hawajitambui tunaomba viongozi wetu waweze kuwa na utaratibu wa kutembelea maeneo yetu ili na wao wajitambue kama nao ni wananchi na ni watanzania,”alisema.

Naye Alhaji Msii ambaye ni mwanachama wa CCWT, alisema kuwa ongezeko la bajeti hiyo litawasaidia wafugaji katika kuondoa migogoro baina ya wafugaji na wakulima.

“Nia ya serikali ni kupima maeneo kwaajili ya wafugaji kitu ambacho kitaondosha kabisa matatizo ya wafugaji na wakulima, kwasababu kutakuwa na maeneo ya wafugaji na maeneo ya wakulima,”alisema.

Kadhalika alisema kuwa fedha hizo zikiwafikia wafugaji matatizo makubwa kwa wafugaji hayatakuepo na badala yake wafugaji wataweza kunufaika na kuendelea kuongeza jitihada katika shughuli zao.