Skip to content

Madereva washauri sheria ya usalama barabarani iandaliwe kwa lugha ya kiswahili

NA TATU MAKAME 

MADEREVA na makondakta wameitaka Mamlaka ya Usafiri na usalama barabarani kuifanyia marekebisho sheria   7 ya 2003 na kuiandika kwa lugha ya Kiswahili, ili na madereva waifahamu na kutumia ipasavyo wakati wanapokuwa katika harakati zao.

Wakizungumza katika mkutano wa elimu ya usalama barabarani ulioandaliwa na Mamlaka hiyo ikiwa ni wiki ya usalama barabarani uliofanyika Raha leo Wilaya ya Mjini.

Madereva hao walisema licha ya kupatiwa elimu ya usalama barabarani lakini bado sheria imeandikwa kwa lugha ya kiingreza ambayo madereva wengi hawaifahamu na kueleza kuwa ndio chanzo cha madereva kutofuata sheria.

Abdalla Khamis Saleh, ambae ni miongoni mwa madereva katika Mkoa wa Mjini Magharib, alisema kuwepo kwa sheria hiyo ya kiingereza imekiwa kikwazo kwa madereva cha kutojua kwa kina sheria za usalama barabarani na kuendelea gari bila kufuata sheria.

“Sheria ya usalama barabarani bado imeandikwa kwa lugha ya kiingreza hata tukitaka kufuata sheria hatujui kwa kina kilichoandikwa ndani yake na madereva wanabakia kufanya makosa”, alisema.

Saleh Abdulla Saleh, ambae ni dereva wa gari za abiria aliitaka Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani, kuharakisha kufanya marekebisho sheria hiyo ili kila dereva na kondakta ajuwe majukumu yake.

“Tunapatiwa elimu lakini kama na sheria wenyewe ingeandikwa kwa lugha ya kiswahili kila mmoja atajifunza kanuni, sheria na kufuata sheria za usalama barabarani”, alisema.

Kwa upande wake Ofisa uhusiano wa Mamlaka ya Usafiri na usalama Barabarani Hakimu Daudi Mwita, alisema Mamlaka inampango wa kuifanyia marekebisho sheria ya mamlaka hiyo, ili kila dereva na kondakta ajue wajibu wake wakati anapoendesha vyombo vya moto.

Awali akifungua mafunzo ya usalama barabarani Mkuu wa kikosi cha Barabarani Mkoa wa Mjini Magharib, Hamis Mwakanolo, aliwataka madereva kufuata sheria za wakati wanapoendesha vyombo vya moto kujikinga na ajali zisizo kuwa za lazima kutokana na kuongezeka ajali kila uchao.

Mapema Mkuu wa kituo cha kikanda cha umahiri katika usalama barabarani kutoka Chuo cha Taifa cha usafirishaji Godlisten Msumanje aliwataka madereva kuacha mazoea wakati wa kuendesha gari na kuangalia vihatarishi vinavyosababisha ajali na kupunguza mwendo kasi ili kupunguza ajali.